Sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu, watumishi tulioitumikia KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa jinsi anavyoendelea kututunza na kutubariki katika maisha yetu.Tunaamini kwamba katika historia imekuwa jambo la kipekee kuweza kukutana na kukaa kwa faragha pamoja na uongozi mzima wa Dayosisi yetu. Kwa hakika imekuwa nafasi muhimu lakini adhimu.

Tunayo kumbukumbu kwamba uongozi uliopo madarakani kwa sasa uliingia madarakani kuiongoza Dayosisi yetu katika kipindi kigumu sana, hasa tukizingatia mambo kadhaa ya msingi:

1.Ni kipindi ambacho Dayosisi ilikuwa imegawanyika sana

2.Waumini wa Dayosisi hii, walikuwa katika hali ya kukata tamaa kiasi cha baadhi yao kuwa wameihama Dayosisi yetu.

3.Sharika zetu na Dayosisi yetu kuonekana kutokuwa na mwelekeo thabiti.

4.Wachungaji, Mashemasi na waumini kugawanyika na hivyo kutoaminiana.

Hali hii imeufanya uongozi mpya wa Dayosisi uliopo madarakani kuwa na kazi ngumu ya mahali pa kuanzia, ingawa tunamshukuru Mungu kwa Neema yake kwa kuupa uongozi mpya Neema ya kuyaona hayo na kuamua kuanza kuchukua hatua nzuri na madhubuti kuiweka Dayosisi yetu katika mstari kwa kutengeneza na kujenga mwelekeo mpya.  Miongoni mwa mambo muhimu tuliyoona yakifanyika ni pamoja na:

  1. Kurudisha mioyo ya waumini waliokata tamaa na mambo ya kiimani

2.Kuona namna ya kurudisha kwa upya uhusiano katika kuaminiwa na Serikali na marafiki zetu.

3.Uongozi wa kujiamini na kujenga moyo wa utayari katika kujitoa kutumika na sio kutumikiwa.

Tumeshuhudia kwa wazi jinsi mwelekeo huo mpya ulivyowekwa wazi katika kutumika kwa nguvu zote na kujenga upya Imani ya waumini na marafiki. Miongoni mwa mambo tuliyoshuhudia ni pamoja na:

  1. Uendelezaji wa miradi ikiwa ni kwa ajili ya kuifanya Dayosisi ilenge kujitegemea katika kipindi kijacho. Tunaona miradi ya vibanda vya biashara, kilimo, na kadhalika.

Kazi hizi zinazofanyika na nyingine nyingi zinazotazamiwa zinachagiza mchango mkubwa kwa maendeleo ya haraka ya Dayosisi yetu kurudi katika mstari kwa upya.  Imani yetu ni kwamba, mambo haya yatairudisha Dayosisi yetu mahali pake.

Kwa ajili hiyo sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu, tuliokutana hapa KOTETI tarehe 28 hadi 29 Novemba, katika mwaka wa Bwana wetu, tunatumia nafasi hii kuupongeza uongozi Mpya wa Dayosisi yetu, kwa kipekee kinara mapambano ambaye ni Mheshimiwa Baba Askofu Dr. Msafiri Joseph Mbilu.  Sisi Wachungaji na Mashemasi Wastaafu tunaweka ahadi kwake kwamba tutaendelea kumwombea afya njema na kumsaidia. Aidha tunamwambia kwamba kustaafu sio kuacha utumishi ila kustaafu ni kuwa uwanja mpya wa mapambano ya kiutumishi.

            Ni sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu

            Tumeitoa leo tarehe 29 Novemba, 2023.

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amesema katika uongozi wake ataendelea kutambua mchango na kazi kubwa iliyofanywa na Wachungaji, Mashemasi pamoja na watumishi wengine waliostaafu ambao  walioitumikia Dayosisi kwa nyakati tofauti na  kuongeza kuwa pamoja na kustaafu utumishi wao bado wanao mchango wa uzoefu , ujuzi na uwezo wa kushauri ili kuondoa makosa katika utendaji.

Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ameyasema hayo tarehe 28.11.2023 kwenye ufunguzi wa kikao chake na Wachungaji pamoja na Mashemasi Wastaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin William  Mkapa Auditorium, uliopo katika, Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) Magamba Lushoto Tanga ambacho kitafanyika kwa siku mbili ambapo kitahitimishwa tarehe 29.11.2023.

Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu ameweka wazi kuwa wastaafu hao watapewa taarifa kutoka Kurugenzi ya Misioni na Uinjilisti,Kurugenzi ya Huduma za Jamii, Kurugenzi ya Uchumi na Mipango pamoja na Kurugenzi ya Fedha na Utawala ili wastaafu hao wapate nafasi ya kutoa maoni na ushauri wao.

Kwa upande wao Mch. Mstaafu Nkhanileka Chedi, Mch. Mstaafu Zawadiel Mkilindi pamoja na Mch. Mstaafu Yohana Mmaka wamesema wamefurahi kwa kupata nafasi ya kukumbukwa na Baba Askofu Dkt.Mbilu kama wastaafu nakuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuitumikia Dayosisi pamoja na kushauri juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Dayosisi.

Kikao hicho kitaangazia kazi za maendelo ikiwemo miradi mbalimbali inayotekelezwa na Dayosisi pamoja na kuwasilishwa kwa taarifa  ya maendeleo ya Shamba la Irente Farm, Taasisi ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) na Ujenzi wa vibanda vya biashara unaoendelea ndani ya Dayosisi.

MATUKIO KATIKA PICHA: Askofu wa KKKT -Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, Tarehe 25/11/2023 akiwa katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Mtonga aliongoza Ibada iliyokuwa na tendo la kuwabariki Vijana wa Kipaimara,Ibada hiyo ilitanguliwa na ufunguzi wa nyumba ya mtumishi.

Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, unatoa pole kwa Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini,kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Erasto Kweka, kilichotokea tarehe:25/11/2023.

Uongozi unatoa pole kwa familia, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini ,Wakuu wa Majimbo wa Dayosisi ya Kaskazini, Wakuu wa Idara zote  za Dayosisi Wachungaji wote wa Dayosisi ya Kaskazini pamoja na  Washarika wote wa Dayosisi ya Kaskazini.

 BWANA ametoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.