Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema (Mt. 28:5-6).

Wapendwa katika Bwana, kufufuka kwa Yesu ni tukio la imani kubwa kwetu sote tunaoamini juu ya nguvu ya ufufuo. Tukio hili linaondoa hofu inayotanda mioyoni mwa wengi juu ya kifo na nguvu ya mauti.

Tunasherehekea Pasaka wakati ambapo mioyo ya wengi imejawa na hofu kubwa ya magonjwa ya kutisha yanayosikika mahali pote duniani, misiba ya kutisha ya kuondokewa na wapendwa wetu. Haya yote yanatuletea mahangaiko na majonzi.

Katikati ya haya yote tunapokea ujumbe mkubwa wa matumaini Malaika anaposema “msiogope”.Tangazo hili la Malaika la kutuondolea hofu linaleta tumaini kubwa kwamba yupo mtangulizi ambaye ameshinda kifo na nguvu ya mauti. Yesu mfufuka analeta tumaini la kutokuogopa kifo na nguvu ya mauti kwetu tunaoamini. Kufufuka kwake hakujatokea kwa bahati mbaya bali ni mpango kamili wa Mungu katika historia ya ukombozi wetu sisi wanadamu. Hii ndiyo maana malaika anakiri akisema “amefufuka kama alivyosema”.

Tuitegemee nguvu ya Mungu iliyomfufua Yesu kuwa sasa tunaye mshindi aliyetutangulia na kwamba sisi sote tunaomwamini hatuna sababu ya hofu ya mauti kwani Bwana amefufuka kutoka kwa wafu.

Huyu Yesu aliyefufuka akaendelee kutujaza matumaini mapya, kwetu mmoja mmoja, matumaini katika familia zetu na jamii kwa ujumla.

 

....................................................................................