Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe.Januari Lugangika ametoa wito kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kupitia Dayosisi zake 26 kuweka kipaumbele kwenye agenda ya kukifufua Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) kwani licha ya Chuo hicho kuwa na sifa ya kutoa taaluma bora na ya kipekee kimekuwa ni alama ya utume wa Kanisa kwa jamii.

Mhe.Lugangika ametoa rai hiyo leo 17/4/2021 alipo kuwa mgeni rasmi kwenye Harambee kubwa awamu ya kwanza iliyo fanyika kwenye ukumbi wa mikutano katika Chuo kikuu cha SEKOMU LUSHOTO. Kwenye harambee hiyo Mkuu wa wilaya amechangia kiasi cha shilingi Milioni mbili.

Mhe.Lugangika amesema wakati rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan alipo tambulisha salamu ya kitaifa inayohamasisha kazi za ujenzi wa taifa kuendelea, ni dhahiri Chuo cha SEKOMU sasa kinapaswa kusimama ili shughuli za uzalishaji zilizo simama zirejee kwa ajili ya manufaa ya wakazi wa Lushoto.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto Bi.Ikupa Mwasyoge aliyekuwa ameambatana na Afisa mipango wa Halmashauri hiyo Bw.Jastine Njuu amesema kuwa Chuo cha SEKOMU kilikuwa chachu ya maedeleo na chanzo kizuri cha mapato kwa wananchi.

Awali Askofu Mteule wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch.Dkt.Msafiri Joseph Mbilu amesema kuwa zipo jitihada mbalimbali zinazo endelea kufanyika kwa kuwashirikisha wana Dayosisi wote waliopo ndani na nje pamoja na wadau wengine wa maendeleo, na kwamba hadi sasa michango inaendelea kukusanywa kwanjia ya makadi na kumefanyika harambee kwenye Mikoa ya Dar es salaam, Kilimajaro na  Arusha.

 

Askofu Mteule ameshukuru ngazi mbalimbali za kiserikali, pamoja na wadau wengine kwa jinsi wanavyo endelea kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha Chuo cha SEKOMU kinasimama.

Kilele cha harambee  kwa awamu ya kwanza kitafanyika tarehe 25 Aprili,2021 katika usharika wa Korogwe jimbo la Tambarare kwa  lengo la kukusanya Tsh. Bilioni mbili (2,000,000,000.)