Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewatahadharisha na kuwaonya watu wanao vamia maeneo mbalimbali ya Kanisa kuacha uchokozi mara moja na wasidhani kuwa yeye ni mpole au mnyonge kwani hatasita kufuatilia haki ya maeneo hayo ambayo yanalipiwa kodi na kumilikiwa kisheria na Dayosisi hiyo.

Baba Askofu Dkt. Mbilu alizungumza hayo tarehe 23/05/2021 kwenye ibada ya kumuingiza kazini Mchungaji Anderson Kipande kuwa Mkuu wa Jimbo la Kaskazini Ibada iliyofanyika katika usharika wa Mlalo Hoheni wilayani Lushoto.

Mchungaji Andesron Kipande alichaguliwa katika mkutano Mkuu uliofanyika Kanisa Kuu (Cathedral) Lushoto kati ya Novemba 25 hadi 27 mwaka jana.

Aidha Askofu Dkt. Mbilu aliwataka wachungaji katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kubainisha maeneo yote ambayo yanakabiliwa na migogoro ya ardhi ili kuona namna ya kumaliza migogoro hiyo.

“Tuanze kwa kutaja jambo dogo ambalo limeendelea kuwa kubwa kwa sababu ya ugumu wa mioyo na vichwa vya wale wasio penda kuelewa lile suala la ardhi na maeneo yetu, niombe tu kukueleza Mkuu wa jimbo kwamba jambo hili tumelichukua  na wale wanaovamia maeneo yetu wafahamu kuwa maeneo yale ni ya Dayosisi” alisema Dkt. Mbilu na kuongeza

“Nami nitamke kwamba wasinichokoze, wanapoona mimi ni mtu ninae cheka na kufurahi wanafikiri mimi ni mtu mnyonge, lakini Dayosisi ninayo iongoza  sio ya wanyonge hata kidogo, na kipekee kitendo alicho fanya Mwenyekiti wa kijiji  kukata mti katika eneo la Lwandai nafahamu jambo hili, nashukuru Mheshimiwa diwani yupo hapa ataendelea kusimamia jambo hili pamoja nasi na tutaliingilia kwa ukali sana kwa kushirikisha nguvu ya ndani na ya nje ya Dayosisi na ninashukuru kwa ushirikiano mzuri tunao upata toka  serikalini”

Awali Mchungaji Anderson Kipande Mkuu wa Jimbo la Kaskazini alimuomba Askofu Dkt. Mbilu kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi inayo milikiwa na Usharika wa Mlalo eneo la Lwandai lililo vamiwa na watu ambao wanafanya shughuli za kilimo, pamoja na eneo la Kwemakame Usharika wa Bethlehemu ambalo wavamizi wamejengea uzio wa mabanzi eneo hilo kiasi cha kuzuia mlango wa kuingia Kanisani.

Mbali na maeneo hayo, maeneo mengine ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambayo yanakabiliwa na uvamizi ni pamoja na eneo lililopo kata ya Vuga ambalo wananchi wanaendesha uchimbaji holela wa madini.

 Usharika wa Ngwelo B Bumbuli, Magamba katika Chuo cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa SEKOMU pamoja na eneo la Hospitali ya Songe wilaya ya Kilindi pia yanakabiliwa na uvamizi.

 Baada ya Ibada hiyo, Askofu Dkt. Mbilu alitembelea na kuonana na wanafunzi, walimu pamoja na wafanyakazi wa Shule ya Sekondari  Lwandai inayo milikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki  kwa lengo la kuwasalimu.

Askofu Dkt. Mbilu alionesha kufurahishwa na Idadi ya walimu waliopo shuleni hapo pamoja na mazingira ya shule yakiwa katika hali nzuri ambayo ni rafiki kwaajili ya kujifunzia huku akimpongeza mkuu wa Shule Mch Daniel Mwarabu walimu, pamoja na wa wafanyakazi wa Shule hiyo kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya ili kurudisha heshima na hadhi ya shule ya Lwandai.