Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru walimu pamoja na wafanya kazi wa vituo vya Irente Rainbow School,Irente School for the Blind, pamoja na kituo cha Irente Children’s Home kwa namna wanavyoendelea kuwahudumia watoto katika vituo hivyo.

Askofu Dkt Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 08/06/2021 alipotembelea vituo hivyo vinavyo milikiwa na KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo  imekuwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuchaguliwa na kuingizwa kazini kuiongoza Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

“Endeleeni kuwafundisha na kuwapenda Watoto wetu katika vituo vyetu kwani sehemu hizi zinahitaji upendo wa hali ya juu”, alisema Askofu Dkt Msafiri Mbilu.

Aidha Askofu Dkt. Mbilu ametanabaisha kuwa anatambua changamoto zilizopo katika vituo hivyo anaimani kupitia kurugenzi za Dayosisi changamoto zilizopo zitatafutiwa ufumbuzi ili wafanyakazi waweze kufanya kazi katika mazingira rafiki.

Mwanafunzi Sofia Omari  wa darasa la  Saba Shule ya Wasioona Irente akiandika Zaburi ya 32:8 kwa kutumia A4 frame na sindano ya kuandikia (stylus)

Halikadhalika katika ziara hiyo Mke wa Askofu, Bi Marry Mbilu ametoa zawadi za mafuta,sabuni  na sukari katika vituo hivyo na kuahidi kurudi tena ili kuendelea kushirikishana uzoefu katika  mambo mbalimbali  yanayohusu Elimu,

Kwa upande mwingine Mwalimu Mkuu wa Shule ya Wasioona Irente, Bi.Levina Urassa ameeleza namna serikali inavyoshirikiana na Shule hiyo katika mambo mbalimbali ambapo amesema serikali imewapatia Mashine ya kuchapa maandishi ya Braille(embosser), Computer 1 na karatasi 228 za kuandikia Braille. .Alieleza zaidi kuwa, serikali inasaidia pia upatikanaji wa chakula, matibabu.pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

 

Katika taaluma, shule hii ndani ya miaka mitatu imekuwa ikishika kati ya nafasi ya 4 hadi ya 5 katika shule ambazo zina Watoto chini ya 40 ngazi ya wilaya.Mwalimu Levina Urassa ameahidi kuwa shule hii itaendelea kufanya vizuri zaidi.

Katika ziara hii Baba Askofu aliambatana na Mch.Dkt.William Kopwe ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Huduma za Jamii KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.