Msaidizi wa Askofu KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki , Mch Michael Mlondakweli Kanju yupo ziarani KKKT Dayosisi ya Karagwe ambapo leo tarehe 25/06/2021 ameongoza ibada  ya kufunga mwezi wa sita katika Kanisa Kuu la Lukajange .Akihubiri katika ibada hiyo kutoka kitabu cha Ufunuo wa Yohana 21:4 amesema kuwa kuna mahangaiko ya aina mbalimbali, machozi ya kila namna,maumivu pamoja na magonjwa,na hali ngumu ya maisha. Hii ni hali ya maisha ambayo watu wanapitia. Bwana Yesu anaahidi kwamba atafuta machozi haya na hayatakuwepo tena.  

 Haya ni maneno ya kuonesha kuwa Yesu yupo katika maisha yetu na tukimshika atatushindia, kwani anaondoa maumivu,machozi,mahangaiko na yeye hatatuacha. “Nawaalika wote kutokumuacha yesu kwani ataendelea kuwaonesha njia na kila siku maisha yenu yatajaa matumaini,atawaangazia na ataendelea kuwashindia" ameyasema hayo Msaidizi wa Askofu Mch.Michael Kanju

Ibada hiyo imewakutanisha watumishi wote kutoka ofisi kuu,Watumishi kutoka katika shule ya msingi ya Tegemeo pamoja na wanafunzi wa Shule ya msingi Tegemeo ambayo inamilikiwa na KKKT Dayosisi ya Karagwe.

Mch Michael Mlondakweli Kanju  aliambatana na mwenyeji wake, msaidizi wa Askofu KKKT Dayosisi ya Karagwe  Mch Yared Apolo Wakami,

Mch Michael Mlondakweli Kanju  atakuwa katika Dayosisi ya Karagwe kwa juma moja, lengo likiwa ni kuendelea kujenga undugu, ushirikiano,kushirikishana uzoefu ,kuhamasisha na kuitangaza UEM pamoja na kazi zote zinazofanywa na UEM. Aidha atashirikiana na msaidizi wa Askofu KKKT Dayosisi ya Karagwe  Mch Yared Apolo Wakami,kufanya kazi za Injili na kutembelea miradi iliyofadhiliwa na UEM katika Dayosisi ya Karagwe.

 UEM: United Evangelical Mission ni chama Cha kiinjili Cha kimisioni kilichoanzishwa miaka 25 iliyopita na wamisionari kutoka Ujerumani wa Rhenish na Betheli ambao walifika Africa, na Asia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Dini. Katika Africa walifika katika nchi 7 ambazo ni Tanzania, DR Congo, Africa ya Kusini, Botswana, Cameroon, Namibia na Rwanda kukiwa na madhehebu 15. Katika Tanzania inawakilishwa na Makanisa 4 ya KKKT ambayo ni KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na KKKT Dayosisi ya Karagwe.

Aidha Chama hiki kinashughulika katika nguzo tano ambazo ni Uhusiano/ Undugu, Diakonia, Uinjilishaji, Utetezi pamoja na Maendeleo.