MKUTANO Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), uliofanyika  katika kituo cha Mafunzo cha Wanawake Morogoro ( Morogoro Women Training Centre), umemchagua Askofu Dkt. Fredrick Shoo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Askofu Dkt. Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa KKKT  Dayosisi ya Kaskazini, alipata kura 63 kati ya kura 212 .

Katika uchaguzi huo majina matano yalipitishwa kuwania nafasi hiyo na Askofu Dk. Shoo aliongoza akifuatiwa na Askofu Dk. Stanley wa Kanisa la Angilikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro aliyepata kura 50.

Aliyekuwa anashikilia nafasi ya Uenyekiti ni Askofu Dk. Alinikisya Cheyo wa Kanisa la Moroviani Tanzania, alipata kura 47, Askofu Dk. Mahimbo Mndolwa ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Anglikana alipata kura 29 na Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Mussa Magwesela akipata kura 23.

Baada ya nafasi ya Mwenyekiti kupatikana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Askofu Oscar Mnung’a wa Kanisa la Angilikana Dayosisi ya Newala aliwaongoza wajumbe wa Mkutano huo kupiga kura za Makamu Mwenyekiti wa kwanza.

Katika nafasi hii Askofu Dkt, Hotay alipata kura 86, akifuatiwa na Askofu Dkt. Cheyo (62), Dkt. Mndolwa (40) na Magwesela (22).

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa pili, nafasi hiyo ilichukuliwa na Askofu Dkt. Cheyo aliyepata kura 84.

Dkt. Cheyo aliongoza mbele ya Askofu Dkt. Mndolwa kwa kura (66) na Magwesela kura (57) kati kura 208 zilizopigwa huku moja ikiharibika.

.....................................