Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki leo tarehe 11/07/2021 ameongoza Ibada ya Jumapili iliyokuwa na tendo la kuwabariki vijana wa kipaimara katika Usharika wa Makorora Jimbo la Pwani. Liturgia iliongozwa na Mkuu wa Jimbo la Pwani Mch Thadeus A. Ketto.

Katika Ibada hiyo jumla ya vijana 30, walibarikiwa na  wanne kati yao walibatizwa huku vijana waliopata kipaimara wakitoa kiasi cha Tsh 105,000/= kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za KKKT-Dayosisi ya Kaskani Mashariki katika masuala ya elimu.

Katika risala waliyoisoma kwa Baba Askofu Vijana hao wameahidi kuwa waaminifu katika maisha yao ya kiimani lakini pia kuishi kwa uadilifu katika jamii inayowazunguka na kuwa mfano mwema na kuitetea imani yao, kutunza urithi kama walivyojifunza katika katekisimo ndogo ya Mch. Dkt Martin Luther kupitia misingi mitatu ya Kilutheri 1. Neema tu 2. Kristo tu, 3. Neno tu.

KATIKA MAHUBIRI: Askofu Dkt. Mbilu amesema kuwa katika zama na nyakati tulizo nazo baadhi ya maeneo na makanisa yamekuwa yakitumia vibaya neno la Mungu kwa kupotosha kwa makusudi waumini jambo ambalo sehemu nyingine limepelekea kuvuruga familia na ndoa za watu huku wengine wakiwa wanafanya  miujiza ya uongo ikiwemo ya kufufua wafu.

Amesema vijana wengi wamepotea kwa kudanganywa na watumishi wasio na hofu ya Mungu jambo ambalo linasababisha vijana kutokufanya kazi na kutegemea miujiza ya uongo.

Sambamba na hayo Askofu Dkt,Mbilu amewataka vijana ambao wamepata Kipaimara kufanya kazi kwa bidii huku wakimtumikia Mungu kwa furaha sambamba na kuendelea kumtegemea na kumpenda kwa kujifunza neno lake siku zote.

Halikadhalika Askofu Dkt Mbilu ameahidi kutoa zawadi ya kengele iliyokuwa katika kiwanda cha uchapishaji (Vuga Press Publishing House) kuwa ya Usharika wa Makorora kutokana na ukubwa wake ambao unaendana na hadhi ya Usharika wa Makorora unao ongozwa na Mch Peter Bendera, huku akimtaka Kaimu Katibu Mkuu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazni Mashariki kuandaa taratibu za kufanikisha zoezi hilo.

 

Kwa upande mwingine  Kaimu Katibu Mkuu Mch. Godfrey T. Walalaze pamoja na salamu mbalimbali alizozitoa ameendelea kuwakumbusha Washarika wa Usharika wa Makorora kuchukuwa tahadhari dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Covid 19) juu ya  matumizi sahihi ya namna ya   uvaaji wa  Barakoa, Kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono (Sanitizer), kuzingatia mlo kamili pamoja na kufanya mazoezi ameongeza kuwa kuzingatia hayo na miongozo inayotolewa na Wizara ya Afya wimbi la tatu la maambukizi halitaleta athari.

 

Ibada ilihudhuriwa na Wachungaji, Wainjilisti, Mashemasi, Kwaya, Washarika pamoja na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Usharika wa Makorora.