Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani LWF Askofu Dkt. Pant Filibus Musa (KUSHOTO) akiwa na Askofu Dkt.Msafiri Joseph Mbilu wa KKKT- DKMs

RAIS wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani LWF, ASKOFU Dkt Panti Musa amesema kuwa umoja ulioyakutanisha Makanisa ya Kiinjili ya Kilutheri Tanzania na Kanisa la Kilutheri la Ethiopia Mekane Yesus unapaswa pia kuwa katika ngazi za Sharika katika Nchi hizo na siyo kwa ngazi ya viongozi ili uwe alama ya matumaini kwenye ulimwengu wa sasa.

Askofu Dkt Musa ameyasema hayo wakati akitoa salamu na shukrani kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania baada ya ziara ya Maaskofu 25 na viongozi wengine wa Juu wa Kanisa la Mekane Yesus katika Ibada iliyofanyika Kanisa Kuu Usharika wa Moshi Mjini Dayosisi ya Kaskazini.

Akipokea shukrani hizo Mkuu wa KKKT Askofu Dkt Fredrick Shoo amesema kuwa KKKT itatembea pamoja na Kanisa la Mekane Yesus katika kumtangaza Yesu Kristo na kuhakikisha kuwa Injili inahubiriwa kwa usahihi wake.

Askofu Dkt Shoo ambaye ameongoza Ibada hiyo amesema kuwa ushirikaono katika ya KKKT na Mekane Yesus utazidi kukua na ziara waliyofanya hapa nchini ni mwanzo tu wa Ushirikiano huo.

Akihubiri katika Ibada hiyo Mkuu wa Kanisa la Mekane Yesus Askofu Jonas Dibisa Jonas amesema mambo mengi yanatazamiwa kutoka Makananisa hayo mawili kwa sababu ndiyo makubwa duniani katika madhehebu ya Kilutheri.

ASKOFU DIBISA ameongeza kuwa kuwa Kanisa la Mekane Yesus limepitia changamoto mbalimbali tangu lilipoanzishwa likiwa na waumini 13 mpaka kufikia waumini zaidi ya milioni 10 waliopo sasa.

Akifafanua kuhusu changamoto na magumu ya mwanzo wa Mekane Yesus ASKOFU DIBASA amesema kuwa mateso yanaweza kulifanya Kanisa kukua.

Maaskofu hao kutoka Ethiopia na viongozi wengine wa Kanisa hilo wameondoka leo kurejea makwao.

 

 Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ni miongoni mwa maaskofu walioshiriki katika ziara hii iliowakutanisha maaskofu wa KKKT na maaskofu toka Ethiopian Evangelical Church Mekane Yesus - Ethiopia. katika hoteli ya corridor spring Arusha kati ya tarehe 13-17 Julai,2021 lengo likiwa  ni kubadilishana uzoefu na kujifunza Zaidi.