Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewapongeza wachunguji walio barikiwa mnamo tarehe 30,06,1991 na kuingia katika hudumu ya kichungaji tayari kutumika shambani mwa Bwana.

Askofu Dkt. Mbilu amesema kuwa anatambua kazi kubwa na nzuri zilizofanywa na wachungaji hao katika maeneo mbalimbali ambayo walipangiwa ikiwa ni ndani na nje ya Dayosisi. Pongezi hizo amezitoa hivi karibuni kwenye Ibada ya jumapili iliyokuwa na matukio mbalimbali ikiwi ni pamoja na jubilee ya miaka 30 ya Wachunjaji wanawake KKKT-DKMs

Naye Naibu Mkuu wa Kanisa la Westphalia Nchini Ujerumani na Makamu mwenyekiti wa UEM, Mch. Dkt Ulrich Moeller ambaye ndie aliye hubiri neno la Mungu kutoka kitabu cha Zaburi ya 84 amesema kuwa wanawake wanapaswa kuendelee kuwa katika mstari wa mbele kama watheologia ndani ya Kanisa wakiwa na hamu kubwa zaidi katika mioyo yao   kwa kile ambacho kinategemewa na Kanisa kutoka kwao.

Katika Ibada hiyo Mch.Dkt Moeller alimpongeza Askofu Dkt Mbilu tangu kuchaguliwa na kuingizwa kazini kuiongoza KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo pia alimpa zawadi ya vyombo vya sakramenti kama kiungo na ishara ya umoja katika Kanisa.

Mch.Dkt. Moeller akiwa ziarani KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki alipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali katika Dayosisi ambayo ni Kiwanda cha uchapishaji cha Vuga press Publishing House, Hospital ya Bumbuli pamoja na chuo cha Bumbuli College of Health and Allied Sciences (BUCOHAS), ambapo amejionea kazi mbalimbali zinazofanywa katika vituo hivyo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kati ya UEM na KKKT-DKMs.

Mnamo tarehe 30/06/1991 historia iliandikwa KKKT-Dayosisi ya Kasakazini Mashariki ambapo wachungaji wanawake watatu walibarikiwa na kuingia katika huduma ya kichungaji. Wachungaji hao ni Mch. Dkt. Anneth Munga,  Mch. Sabina Lumwe (Kulia) na Mch. Joyce Kibanga (Kushoto).

Wachungaji hao wanawake wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki wameadhimisha miaka 30 tangu kubarikiwa kuwa Wachungaji, wameungana na mwimba Zaburi ya 32: 8 aliposema “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea: Nitakushauri, jicho langu likikutazama” Wachungaji hao wamekiri kuwa tangu mwaka 1979 KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, ilipowatuma masomoni katika Chuo cha Makumira, mpaka siku hiyo ya  jubilee Mungu hakuacha kuwafundisha, kuwaonyesha njia, kuwashauri na jicho lake likiwatazama.

Mnamo mwaka 1979 KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilichukua uamuzi kupitia vyombo vyake vya maamuzi kupeleka mwanamke wa kwanza kwenda kusomea theolojia katika Chuo cha Uchungaji Makumira. Jambo hili lilikua ni jambo jipya sio tuu kwa Dayosisi yetu bali pia kwa Kanisa zima la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Hii ni kutokana na mapokeo mbalimbali katika kila Dayosisi.

 Haikuwa jambo rahisi kutokana pia na mtazamo wa jamii ilivyokuwa inawachukulia wanawake kutumika katika huduma ya kichungaji ndipo mwaka 1981 Wanawake wengine wawili walipelekwa kujiunga na masono ya Theolojia.

Baada ya kumaliza masomo walipangwa kwenye Sharika kutumika kama Watheolojia.  Hawakufanya mambo ya kichungaji kwa mfano; kutoa Chakula cha Bwana, kufungisha ndoa na ubatizo bali walihusika katika kuongoza Ibada zikiwemo Ibada za mazishi, kufundisha madarasa ya Kipaimara,  kufundisha Elimu ya Kikristo mashuleni, kufundisha wainjilisti na mashemasi na kuongoza idara za akina mama.

Katika kipindi chote hicho mijadala mbalimbali ya kubariki wanawake kuwa wachungaji iliendelea katika Dayosisi na Kanisa kwa ujumla.  Mwaka 1990 Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania katika Mkutano wake Mkuu uliofanyika Morogoro pamoja na mambo mengine walifanya uamuzi wa  kubariki wanawake kuwa wachungaji. Ndipo uhuru ukatolewa kwa Dayosisi zile ambazo zilikuwa  tayari kufanya hivyo.

Mwaka 1991 Juni 30 muda mfupi baada ya uamuzi huo ndipo KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilipoamua kuwabariki wanawake wa kwanza kuwa wachungaji. Ibada ya siku hiyo iliongozwa na Hayati Askofu Dkt. Sebastian Kolowa akishirikiana na Askofu Elinaza Sendoro wa KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Hata hivyo Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki iliwapa fursa wachungaji hawa wanawake ya kufanya kazi kwenye Sharika, Kurugenzi, Idara na Vituo ndani ya Dayosisi na katika KKKT kwa nyakati tofauti.

Siku hiyo Dayosisi ilikuwa pia inahitimisha maadhimisho ya miaka 100 tangu injili ilipoingia KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, pia walibarikiwa watheolojia wanaume kumi na moja.  nao ni   Mch. Lewis Shemkala, Mch.Emmanuel Mtoi, Mch.Nkanileka Chedi, Mch. Abdiel Mdoe, Mch.Vales Kusaga, Mch. Eliapenda Njuga, Mch. Christian Kolowa, Mch. Samwel Hozza, Mch. Zefania Kasinda, Mch. Togolai Shelukindo pamoja na Mch. Aseri Majoh.

Miongoni mwa hawa waliobarikiwa wafuatao wametangulia mbinguni, nao ni Mch. Samwel Hozza, Mch. Zefania Kasinda, Mch. Togolai Shelukindo pamoja na Mch. Aseri Majoh.

 Hata hivyo Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki iliwapa fursa wachungaji hawa wanawake ya kufanya kazi kwenye sharika, kurugenzi, idara na vituo ndani ya Dayosisi na katika KKKT kwa nyakati tofauti.