Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo amewataka Wakristo kuwa mstari wa mbele katika kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Nchini Agosti 23 mwaka huu na kuwahimiza Wachungaji na Mashemasi kuendelea kuwakumbusha waumini mara kwa mara kujiandaa na zoezi hilo.

Askofu Dkt. Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) amesema kuwa zoezi hilo litasaidia kuweza kupata idadi sahihi ya wananchi itakayo isaidia  serikali katika mipango yake mbalimbali ya sasa naya baadae.

Mkuu wa KKKT ameyasema hayo leo tarehe 30/07/2022 wakati akitoa salamu zake kabla ya Mahubiri kwenye Ibada ya kuwabariki vijana wa Kipaimara 21 miongoni mwao wawili walibatizwa iliyofanyika Usharika wa Makorora, Jimbo la Pwani ambako anaendelea na ziara yake rasmi ya kikazi.

Pamoja na hayo Askofu Dkt. Shoo amelikumbusha Kanisa kuendelea kuiombea nchi kama lifanyavyo katika sala kuu kila Ibada ya Jumapili, kuombea uongozi wake na Rais Samia Suluhu Hassan i ili Mungu aendelee kuwajaza hekima, afya njema, ujasiri, moyo wa huruma na upendo.Amesema viongozi wakipata baraka hizo nchi itabarikiwa, haki na mshikamano utaendelea kuwepo kwa watu wote.

Awali Kabla ya Ibada Mkuu wa Kanisa aliweka jiwe la msingi la Kanisa hilo la Makorora ambapo kwa upande wake Askofu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru wote waliojitolea kukamilisha ujenzi huo akiwemo Waziri wa Nishati ambae pia ni Mbunge wa Bumbuli Mhe. Januari Makamba.

Mara baada ya Ibada hii msafara wa Mkuu wa KKKT umerejea Wilayani Lushoto yalipo Makao Makuu ya KKKT-DKMs ambapo kesho tarehe 31/07/022 Askofu Dkt. Shoo majira ya asubuhi ataongoza Ibada ya jumapili katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto na baadae mchana atatembelea vituo vya Irente Rainbow School, Irente Children’s Home, Irente School for the Blind na Irente Farm.

Mkuu wa Kanisa atahitimisha ziara yake siku ya tarehe 01/08/2022 katika Jimbo la Kaskazini (Mlalo) ambapo pia kutafanyika Ibada katika Usharika wa Mlalo na majira ya mchana ataelekea katika Shule ya Sekondari Lwandai ambapo Baba Askofu Dkt. Shoo atafungua Jengo la Maabara ambalo lilifanyiwa ukarabati mkubwa na majira ya jioni msafara wa Mkuu wa Kanisa utaelekea katika Chuo Kikuu kitarajiwa cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI).