Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt. Fredick Onael Shoo amewaasa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lwandai inayomilikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kusoma kwa bidii na kumtanguliza Mungu katika masomo yao ili kutimiza ndoto zao.

Ameyasema hayo leo tarehe 01/08/2022  akihitimisha  ziara yake ya siku 6 ndani ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika Jimbo la Kaskazini wakati wa ufunguzi wa maabara ya kujifunzia masomo kwa vitendo ambayo imefanyiwa ukarabati mkubwa katika Shule ya Sekondari Lwandai, huku akifurahishwa na matokea mazuri  na kuahidi kuwa balozi wa Shule hiyo.

Askofu Dkt. Shoo pia ameupongeza uongozi wa Dayosisi chini ya Askofu Dkt. Joseph Mbilu, kwa jitihada mbalimbali zilizofanywa na uongozi kwa kuanza kurudisha uhai katika Shule hiyo hivyo kuwa na matumaini kuwa shule hiyo itakuwa ni moja ya Shule bora kitaifa.  

Kwa upande wake Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt Msafiri Joseph Mbilu amesema kuwa Mlalo ndio kitovu cha Dayosisi  na kusisitiza kuwa wapo watumishi mbalimbali ambao wamezaliwa na wengine kutumika katika Usharika wa Mlalo  sambamba na kusema kuwa Shule ya Lwandai imekuwa na historia kubwa kwakuwa ndipo ilipoanzia Shule ya Sekondari Eliboru na Chuo kikuu cha Makumira.

Nae Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashidi Shangazi ameahidi  kushirikiana na Kanisa katika mambo mbalimbali yanayohitaji msaada kutoka serikalini  ili kupata msaada wa haraka sambamba na  kushukuru Kanisa kwa kutoa huduma muhimu kwa jamii ikiwemo mashule Hospitali na vituo vya huduma ambavyo kipekee vinamilikiwa na Kanisa.

Ikumbukwe kuwa ziara  ya mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania  katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilianza tarehe 27/7/2022 na kuhitimishwa tarehe 01/08/2022 ambapo katika ziara hiyo ametembelea sharika na vituo mbalimbali vya huduma pamoja na kuweka  mawe ya msingi katika Sharika za Dayosisi. Hapo kesho Mkuu wa KKKT atapata nafasi ya kuagana na mwenyeji wake Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ndipo atakapo rejea katika majukumu yake.