Print

 

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameipongeza Bodi inayosimamia Zahanati ya Mtae Mission  pamoja na Washarika wa Usharika huo kwa juhudi walizozifanya na kupelekea zahanati hiyo kufunguliwa tena kwa upya 

ambayo itakwenda kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa eneo.

ASKOFU DKT. MBILU AKIKATA UTEMBE ISHARA YA UZINDUZI WA MNARA WA KENGELE USHARIKA WA  MTAE MTAA WA MAMBO

Pongezi hizo amezitoa leo akiwa katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Mtae kwenye Ibada ya Jumapili iliyokuwa na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa Mnara wa kengele katika Usharika wa Mtae Mtaa wa Mambo,kufunguliwa kwa Upya Zahanati ya Mtae pamoja na tendo la kuwabariki vijana wa kipaimara ambapo amesema zahanati hiyo ni Muhimu kwa wanamtae na kuipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Aidha Askofu Dkt. Mbilu amesema kufunguliwa kwa upya zahanati hiyo ni kutunza  heshima ya Usharika wa Mtae na Dayosisi kwa ujumla, na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya Afya katika eneo hilo ambapo awali wananchi walilazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Wilaya  Lushoto.

Kadhalika Askofu Dkt. Mbilu amesema azma ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ni pamoja na kutoa huduma za kiroho na za kimwili ikiwemo zahanati hiyo  iliyoanzishwa mwaka 1926 kuwahudumia watu wote tena kwa upendo pindi wanapofika kupatiwa matibabu na hivyo kuitaka bodi ya zahanati hiyo kutokuwa sababu yoyote itakayo pelekea kufungwa tena kwa zahanati hiyo.Katika Ibada hiyo jumla ya vijana wapatao 90 wamebarikiwa na watatu kati yao kubatizwa.

Katika Hatua Nyingine Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa wazazi, walezi na watu wote wanaopenda kujiunga na kozi ya Pharmacy katika ngazi ya Certificate na Diploma kwenye Chuo cha Kolowa Technical Training Institute  chenye usajili namba KOTETI/HAS/249, kutuma maombi kwa kupitia mfumo wa (CAS)  kwenye tovuti ya NACTE  ambapo dirisha la awamu ya pili la Udahili wa pamoja kwa kozi za Afya litafunguliwa hapo kesho tarehe 15 Agosti,2022.

Chuo hiki kipo Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga na kitatumia majengo ya kilichokuwa Chuo Kikuu cha SEKOMU. 

Hits: 7590