Mchango wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kuelekea uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi - KIGOMA HAPO KESHO TAREHE 09/10/2022.

Wakristo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, waliokuwa wanafanya kazi Mkoani Kigoma, walijikusanya chini ya uongozi wa ndugu. Edward Kiswaga aliyekuwa mtumishi wa Uhamiaji. Waliandika barua yao Makao Makuu ya KKKT yaliyopo Mkoani Arusha kuomba wapatiwe Mchungaji atakaye wahudumia kwa taratibu za Kilutheri.

Wakati huo walikuwa wakijiongoza wenyewe wakisali katika chumba cha darasa katika shule ya msingi Muungano iliyoko Mwanga Kigoma. Kabla ya hapo walikuwa wakipewa huduma za kiroho na Mchungaji wa Kanisa la Moravian Kigoma.

Mkuu wa KKKT Hayati Askofu Dkt. Sebastian Kolowa na Katibu Mkuu wa KKKT ndugu. Joel Ngeiyamu wakati huo walipokea ombi la washarika wa Kilutheri Kigoma na kulipeleka kwa Halmashauri Kuu ya KKKT. Uamuzi wa Halmashauri Kuu ya KKKT ulikuwa kukabidhi Misioni ya Kigoma itunzwe na Dayosisi tatu zifuatazo kwa kupokezana kila baada ya miezi mitatu.

  • KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki
  • KKKT-Dayosisi ya pare
  • KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.

KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilikuwa ya kwanza kuitikia haraka wito wa KKKT na kumtuma Mchungaji kigoma. Tarehe 4/4/1983 Mchungaji Msaidizi Zawadiel Joseph Mkilindi alibarikiwa kuwa Mchungaji katika Kanisa dogo la Usharika wa Lushoto na kutumwa Mkoani Kigoma.Mchungaji Zawadiel Joseph Mkilindi alikabidhiwa Usharika wa Kigoma na Katibu wa Misioni na Uinjilisti wa KKKT-DKMs Mch. Timilai Ismael Guga, katika Ibada iliyofanyika katika darasa la shule ya msingi muungano katika manispaa ya Kigoma Ujiji. Wakati huo Usharika ulikuwa na mitaa mitatu ambayo ni:- Kigoma mjini ,Kagunga Kaseke. Aidha palikuwa na kikundi cha kwaya ya vijana Kigoma Mjini.

WITO WA MAFUNDISHO YA UWAKILI NA KUJITEGEMEA.

Mchungaji Mkilindi aliwatia moyo Washarika wa Kigoma kwa kuweka mambo matatu mbele yao ambayo ni ya mkazo wa mafundishi ya uwakili na kujitegemea. Kwa kuinua moyo wa umoja, kujitoa na kujitolea kujenga ufalme wa Mungu kwa kutoa mali na vipawa vyao kwa hali ya juu; uinjilisti uliwezesha falsafa iliyosaidia kuendeleza kazi ya Bwana na kusaidia kusimama katika mambo matatu: - Kujitegemea- Self Reliance, Kujiongoza – Self Governing pamoja na Kujieneza - Self Propagation.

falsafa hii ilisaidia Washarika kujua kuwa kazi ya mungu iko mikononi mwao. hivyo watumie mali, hazina na vipaji vyao kujenga na kueneza ufalme wa mungu Mt. 28: 19-20, Mk 16:15.

Hata hivyo Mch Zawadiel Mkilindi kazi yake ya kwanza ilikuwa kuwatembelea wakristo kwa miguu majumbani na maofisini ili kufahamiana na kuwaimarisha kiroho, alitembea katika maeneo ya biashara ili wafanyabiashara nao wafike Kanisani. Ziara hizi zilijenga umoja na mshikamano katika Yesu Kristo na kupanua wigo wa mahudhurio Ibadani.

Huyu ndiye mmisionari wa kwanza wa KKKT-KIGOMA Mch Zawadiel Joseph Mkilindi.