Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu leo tarehe 15/10/2022 akiwa katika Jimbo la Kaskazini Usharika wa Kireti Mtaa wa Mp'anda, ameongoza maombi maalum ya kumshukuru Mungu kufuatia kufunguliwa kwa Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kinacho milikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa Wachungaji, Mashemasi, Wainjilisti kuweka mpango wa maombi  ya kumshukuru Mungu kwenye Sharika, Mitaa yote na hata ngazi ya familia  kuanzia kesho hadi tarehe 31 ya mwezi Octoba 2022 kwa kuzingatia mambo yafuatayo, Kumshukuru Mungu kwa kufunguliwa kwa Chuo cha KOTETI, Kumuomba Mungu akitunze,kukilinda na kukikuza  Chuo hicho ili kidumu na  kuwa Chuo kizuri kitakacho wavutia wengi katika nyanja mbalimbali za maisha na mwisho kumuomba mungu aendelee kututia nguvu  katika kuchangia deni la Dayosisi hadi litakapo fika mwisho.

Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu amewatahadharisha waliopewa majukumu ya kukisimamia chuo hicho kuwa makini kwa kila jambo wanalo lifanya ili makosa yaliyo jitokeza huko nyuma kwenye kilichokuwa Chuo cha SEKOMU hayajitokezi tena kwa namna yoyote ile.

Chuo cha KOTETI kwa sasa kinaendelea kupokea wanafunzi tayari kuanza mhula wa masomo Kozi ya Ufamasia (Pharmacy) inahusika na uandaaji, kuchanganya na kutoa dawa za kimatibabu kwenye mahospitali, maduka ya madawa, na viwandani na Vigezo vya kusoma kozi hii ni kuanzia ufaulu wa "D" kwenye masomo ya Chemistry na Biology na "D" nyingine 2 kutoka kwenye masomo mengine mawili kidato cha NNE yasiyo ya Dini. Baadae Chuo hiki kitaongeza kozi mbalimbali. Chuo kipo MAGAMBA katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga www.koteti.ac.tz.

Muonekano wa Kanisa la Mtaa wa Mp'anda

Hata hivyo Baba Askofu Dkt. Mbilu ameongoza Ibada ya kipaimara pamoja na kuweka jiwe la msingi la Kanisa na kulifungua Kanisa la Mtaa wa Mpanda.Katika Ibada ya Kipaimara jumla ya vijana 138 walibarikiwa. Waliobatizwa katika Ibada hiyo ni watu wazima 11 na watoto 2.