Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa namna walivyo jitoa kwa hali na mali katika kufanikisha uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi.Shukrani hizo amezitoa leo tarehe 16/10/2022 wakati akihubiri kwenye Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Jimbo la Kusini Usharika wa Bumbuli.

Dayosisi hii ya Magharibi inakuwa ya 27 ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania awali ilitambulika kama Misioni ya Kigoma na KKKT-Dayosisi ya Kaskazni Mashariki ikiwa mlezi wa iliyokuwa Misioni hiyo. Baba Askofu Dkt. Mbilu  na msafara wake walishiriki kwenye Ibada ya uzinduzi wa Dayosisi hiyo iliyofanyika Jumapili  ya tarehe 09/10/2022 ikiwa na matendo makuu ya   kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini kwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Magharibi Baba Askofu Jackson Amala Mushendwa. 

Hata hivyo Baba Askofu Dkt. Mbilu amewashukuru wanadayosisi kwa namna wanavyoendelea kujitoa na kuchangia deni la Dayosisi ambapo kupitia michango hiyo  matunda yameanza kuonekana ikiwemo kufunguliwa kwa  Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI).

Aidha katika Ibada hiyo  iliyokuwa ya baraka kulikuwa na tendo la kuwabariki vijana wa Kipaimara ambapo jumla ya vijana 159 walibarikiwa na 2 miongoni mwao walibatizwa.

Kwa upande wa viongozi wa Ibada Mkuu wa Jimbo la Kusini Mch. Issai Mweta aliongoza Liturgia katika sehemu ya kwanza ya Ibada hiyo na katika sehemu ya pili ya Ibada ya kuwabariki vijana wa kipaimara iliongozwa na Mch. Alice Kopwe.

Hata hivyo katika mahubiri ya Baba Askofu Dkt. Mbilu amewasihi waumini kutovutwa na mafundisho potofu ya neno la Mungu yaliyojaa utapeli, bali wajikite katika kuisimamia imani ya kweli na kukumbuka upendo wa kweli wa Mungu kupitia mwana wake Yesu Kristo pamoja na neno la mahubiri lililosomwa kutoka katika kitabu cha Injili ya Luka Mtakatifu 7:11-17 masomo mengine ni Zaburi ya 131:1-3. kichwa kinachoongoza juma hili kinasema UPENDO WA KWELI WATOKA KWA MUNGU.