Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini  Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameonyesha kuridhishwa na hali na mwenendo mzuri wa Shule ya Sekondari ya Lwandai na kuwapongezi walimu na wafanyakazi wa Shule hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kurejesha heshima ya Shule hiyo kongwe hapa Nchini.

Akizungumza kwenye mahafali ya 33 ya kidato cha nne yaliyofanyika leo tarehe 22/10/2022 katika shule hiyo  ameeleza kuwa matokeo mazuri yanayoendelea kupatikana Shuleni hapo ndiyo yatakayo endelea kurudisha imani ya wazazi na walezi kwa shule hiyo huku akifurahishwa na namna ya wanafunzi hao wanavyo weza kujieleza hasa kwa kutumia Lugha ya kiingereza.

Amewasihi wahitimu hao kuitumia vema elimu waliyoipata ili ileta tija kwa taifa. Askofu Dkt. Mbilu ameuhakikishia uongozi wa Shule hiyo kuwa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki  mmiliki wa Shule hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa shule hiyo.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika shule hiyo hivi karibuni  ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu pamoja na maboresho mbalimbali katika miundumbinu ya Shule inayochangia ukuaji wa taaluma kwa vitendo ikiwemo maabara ya shule hiyo kukarabatiwa na kuongezewa ubora unaowasaidia wanafunzi kisaikolojia na kupenda masomo ya sayansi.

Mazazi rasmi, Mwl. Neema Msumali

Mahafali haya yalifana sana yakipambwa na vishirikisho mbalimbali, maonesho na nyimbo kutoka kwa wahitimu na wanafunzi wengine.mazazi rasmi katika mahafali haya alikuwa Mwl. Neema Msumali .

Sehemu ya Risala iliyosomwa kwa Baba Askofu na wanafunzi Ally Mohamed Mhando pamoja  na  Salha Salehe Kaoneka imeeleza kuwa, mafanikio mengi shuleni hapo  ni kutokana  na maboresho mbalimbali katika miundo mbinu ya Shule inayochangia ukuaji wa taaluma kwa vitendo,chini ya uongozi wa Mkuu wa Shule Mch. Danieli Mwarabu mwenye maono makubwa ambaye amesababisha maabara kukarabatiwa kwa kuongezewa ubora unaowasaidia wanafunzi  kupenda masomo ya sayansi.

Vilevile wanafunzi hushiriki elimu kwa vitendo katika kulima mbogamboga, kufuga kuku na samaki elimu ambayo imewasaidia kupata ujuzi wa kujitegemea katika maisha.

Miradi hii imewafanya kushiriki kikamilifu katika kufanya kazi za mikono na kuwajengea ukakamavu na kuwawezesha  kukabiliana na changamoto za maisha baada ya kuhitimu kidato  cha nne. Pia Shule imefanikiwa kuweka miundombinu ya nishati ya umeme wa jua (Solar System) ambao unawasaidia wanafunzi kuendelea na masomo pindi umeme wa gridi ya taifa (TANESCO) unapokatika. 

# Shule ya Sekondari Lwandai sasa inaendelea kupokea wanafunzi wanaohitaji kujiunga na  kozi ya kujiunga na kidato cha kwanza

(PRE – FORM ONE COURSE) kwa mwaka wa masomo 2023 ambapo hadi sasa wanafunzi wapatoa 60 wanaendelea na kozi hiyo.

 Unaweza kupiga 0786066702 /  0 762 629 854 Kwa maelezo zaidi.