"Matengenezo ya Kanisa si jambo la kutokea kwa mara moja hivyo Kanisa linapaswa kuwa katika hali ya matengenezo wakati wote kwa kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu" Askofu Dkt. Fredrick Shoo, Mkuu wa KKKT.

Askofu Dkt. Shoo amezungumza hayo wakati wa Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Dkt. Syprian Hilinti na kumsimika Msaidizi wa Askofu Mch. Dkt Zephania Nkesela katika Kanisa Kuu, KKKT-Dayosisi ya Kati (Singida) leo tarehe 30/10/2022.

Askofu Dkt. Shoo amewataka viongozi hao  kuonyesha njia kwa mfano na mwenendo huku wakitembea kwa pamoja na umoja katika kuliongoza kundi ambalo wamepewa na Mungu kuliongoza.

" Sina mashaka na Dayosisi hii kwa kuwa ninyi ni waasisi wa umoja hivyo muendelee hivyo kwa kumtanguliza Mungu" Askofu Dkt. Fredrick Shoo

Mkuu wa KKKT Askofu Dkt. Shoo amewaasa Wakristo kuepuka mafundisho mengi ya sasa ambayo ni potofu ambapo wengi hufuata miujiza bali wanapaswa kulisoma, kuliamini na kuliishi Neno la Mungu ili waone nguvu ya Mungu katika maisha yao.

MKUU WA MKOA WA SINGIDA MHE. PETER SERUKAMBA

Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Peter Serukamba (akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Samia Suluhu Hassan) amesema Serikali inatambua mchango wa Kanisa katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii kama vile Afya na Elimu na kuahidi kutatua changamoto mbalimbali zilizotolewa na Askofu Dkt. Hilinti wakati wa hotuba yake.

Askofu Dkt. Syprian Hilinti anakuwa Askofu wa tano (5) wa KKKT-Dayosisi ya Kati (Singida) ambaye ataongoza Dayosisi hiyo kwa kipindi cha miaka 10.

Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu (WA KWANZA KULIA) ni miongoni mwa maaskofu walioongoza sehemu ya pili ya Ibada hiyo ya kumuweka wakfu Baba Askofu Dkt. Syprian.