Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewapongeza Wanawake wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki hususani Wanawake wa Usharika wa Irente kwa mambo makubwa wanayoendelea kuyafanya katika Dayosisi.
Wanawake hao wamepongezwa kutokana na kuuenzi mwaka wa Wanawake na kuwataka kuendelea kufanya hivyo ili mwaka wao ujioneshe na kujitambulisha wenyewe kwa kazi mbalimbali wanazozifanya na watakazoendelea kuzifanya.
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo tarehe 19/11/2022 akiwa kwenye Kongamano la maonyesho ya kazi za Wanawake katika Jimbo la Kusini, Usharika wa Irente ambao waliandaa maonyesho ya vitu mbalimbali wanavyo vitengeneza huku akiwaasa kuamka na kuchukuwa nafasi ya utumishi kutumika katika jamii,Kanisa na Taifa kwa ujumla kwa vipawa walivyo pewa na Mungu.
Askofu Dkt. Mbilu hakusita kuzitaka Sharika nyingine kuiga namna Wanawake wa Usharika wa Irente walivyo adhimisha mwaka wa Wanawake katika ngazi ya Usharika kwa vitendo.

Ikumbukwe kuwa kupitia Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazani Mashariki kwa kauli moja ilipitisha  mwaka 2022 uwe mwaka wa Wanawake katika Dayosisi huku ukiongozwa na kauli mbiu kutoka kitabu cha Waamuzi 5:12a: - Amka ,Amka ,Debora; Amka,amka, imba wimbo.

Wanawake wa Usharika huo wamemshukuru kipekee Baba Askofu kwa kuacha shughuli zake na kuungana nao katika kuadhimisha siku ya kongamano la wanawake katika Usharika huo.

“Ndugu mgeni rasmi tunaishukuru Dayosisi yetu kuufanya mwaka 2022 kuwa mwaka wa Wanawake kidayosisi, kwani imetusaidia kufahamiana, kushirikiana kutatua changamoto mbalimbali, kutiana moyo kuinuana kiroho pale ambapo tumekata tamaa na kiuchumi”.

Wanawake wa Usharika wa Irente, katika kutimiza malengo mbalimbali waliyojiwekea katika mwaka huu wamefanikiwa kutekeleza mambo yafuatayo :

Kwanza kufanya uzinduzi wa mwaka wa Wanawake kiusharika, kufanya semina ya Wanawake iliyohusu wajibu wa Mwanamke katika Kanisa na jamii kwa ujumla, kuimarisha na kuendeleza kikundi cha VICOBA cha Wanawake usharikani.

Kuendeleza kazi za mikono za Wanawake usharikani na katika jumuiya ambazo ni kama ifuatavyo Mradi wa Nguruwe, Mradi wa batiki, utengenezaji wa kapeti,ususi wa mikeka na vikapu, utengenezaji wa sabuni, usimamiaji  sikukuu za mikaeli na Watoto, maombi ya dunia na maandalizi ya Ibada ya Advent.

Wanawake wa Usharika wa irente pia wameweka alama ya utengenezaji wa Mabenchi 10 (kumi) ya kukalia kama uwekaji wa alama ya kumbukumbu yao ya maadhimisho ya mwaka wa wanawake  2022. Ambapo  leo walikabidhi mabenchi matatu (3) ambayo yapo tayari kutumika huku wakikabidhi payslip ambayo fedha yake imekwisha ingizwa benki kiasi cha Tshs. 100,000 (laki moja tu) kwa ajili ya mchango wao  kukabiliana na deni la Dayosisi.Wameeleza kuwa wanafanya hivyo kuonyesha ni kiasi gani wanaguswa na shida viongozi wao wanayoipata kwa sababu ya madeni makubwa waliyorithishwa toka uongozi uliopita.