Katika picha Askofu  Dkt. Msafri Joseph Mbilu, akiwa na mwenyeji wake Askofu Johan Tyrberg.  Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu yupo ziarani katika Dayosisi ya Lund-Sweden, ziara hii ni mwendelezo wa ziara zake ndani na nje ya nchi zenye   lengo la kuimarisha urafiki pamoja na kujifunza mambo mbalimbali na mengi yatakayo faa kwa ajili ya Dayosisi na Kanisa.

 

KATIKA PICHA: Sehemu ya msafara ulioambatana na Askofu Dkt. Msafiri Mbilu 

Askofu Dkt. Mbilu atapata nafasi ya kutoa taarifa mbalimbali juu ya urafiki na hali ya Dayosisi kwa sasa katika sharika na vituo mbalimbali, atahutubia katika Chuo Kikuu cha Lund (Lund University), pamoja na kukutana na watumishi wa Kanisa na wachungaji. Ziara hii ya Askofu Dkt. Mbilu  inatoa fursa ya kukuza uhusiano na urafiki kati ya Dayosisi hizi.

Askofu Martin Modéus

Jumapili ya tarehe 04/12/2022 Askofu Dkt. Mbilu atamuwakilisha Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo kwenye Ibada ya kuingizwa kazini kwa Mkuu mpya wa  Kanisa la Sweden, Askofu Martin Modéus. 

Askofu Martin Modéus alipata asilimia 59 (59%) ya kura katika uchaguzi  wa Askofu Mkuu uliofanyika tarehe 08/06/2022. Hivyo atakuwa Askofu Mkuu mpya wa Kanisa la Sweden, akimrithi mtangulizi wake Askofu Antje Jackelen, ambaye alistaafu tarehe 30 Oktoba ya mwaka huu. Askofu Modéus ataingizwa kazini kuwa Askofu Mkuu mpya tarehe 4 Desemba 2022.

Askofu  Modéus anakuwa Askofu Mkuu wa 71 wa Kanisa la Sweden katika mlolongo usiokatika tangu Askofu Mkuu wa kwanza, Askofu Stephanus, mwaka 1164. Askofu  Martin Modéus kwa sasa ni Askofu wa Dayosisi ya Linköping.

Ujumbe wa Askofu huyu mpya wa Kanisa la Sweden "Ninashukuru na nina furaha ninatazamia kutekeleza majukumu yangu, kwa msaada wa Mungu na kwa msaada wa wenzangu wazuri na wafanyikazi. Sasa ni wakati wa maandalizi, tafakari na maombi kabla ya kuingizwa kazini,” alisema Askofu Martin Modéus mara baada ya kupokea wajibu huo.