Isaya 9:2 “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”

 Ndugu zangu wapendwa wana KKKT – DKMs, inawasalimu katika Jina la Bwana na Mwokozi wetuYesu Kristo! Heri ya Krismas. Tunamshukuru Mungu Baba yetu wa Mbinguni aliyetujalia sisi sote kuiona Krismass ya mwaka huu 2022.

 Siku hii ni sikukuu ambayo sisi Wakristo tunapokea zawadi kubwa kutoka kwa Mungu mwenyewe kwa kumtoa mwanawe mpendwa Yesu Kristo azaliwe katika ulimwengu huu kwa ajili ya ukombozi wetu.

 Kuzaliwa kwa Yesu ulimwenguni ni alama ya kuingia kwa nuru katikati ya giza nene lililotanda ulimwenguni pote. Nabii Isaya anaungana na Manabii wengine akitabiri ujumbe mkubwa wa matumaini kuwa mwisho wa giza unakaribia katika kuja kwa Masihi wa Bwana, yaani Yesu Kristo.

 Yesu Kristo amekuja ili kuondoa giza lililotanda katika maisha yetu ulimwenguni hapa. limwengu tunaoishi umejawa na aina mbalimbali za giza. Giza la rushwa na roho ya uonevu, giza la vita na mauaji yanayopelekea ugumu wa maisha kwa watu wengi, giza la mauaji ya vikongwe kwa ajili ya imani potofu za ushirikina, giza la mafundisho potofu yanayoletwa na manabii wa uongo wanaolenga kujinufaisha kwa mali za watu, giza la maisha ya anasa na kupenda dhambi

Haya yote yanamhitaji Yesu anayeleta nuru ili iangaze mioyoni mwa watu waikubali nuru hii na kumkaribisha katika maisha yao.

Tuelendelee kumpokea Yesu azaliwe katika maisha yetu ili tulishinde giza na Nuru ya kweli iangaze pote. Yesu anayezaliwa akaendelee kuwa jibu la maombi yetu daima, katika familia zetu na mahali pote.

 Nawatakia Krismasi njema na baraka za Mungu tunapojiandaa kuupokea mwaka mpya wa 2023.

 Ni mimi Mtumishi mwenzenu Shambani mwa Bwana!

 Mch. Dkt. Msafiri Joseph Mbilu

ASKOFU – KKKT -DKMs

 Katika Sikukuu hii Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameongoza Ibada ya Krismasi, Kanisa Kuu Lushoto.