Waziri wa Nishati, na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli Mhe.January Makamba amefika katika Ofisi za Makao Makuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki leo tarehe 03/01/2023 na kutoa salamu zake za Mwaka Mpya, pongezi na shukrani kwa Askofu Dkt Msafiri Joseph Mbilu kwa ushirikiano mkubwa anaouonyesha katika ngazi ya jamii na Serikali kwa ujumla.

 Mhe. January Makamba ameahidi kwamba wao kama viongozi wa Serikali wataendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono juhudi na mipango inayofanywa na KKKT-DKMs na Kanisa kwa ujumla ikiwemo kuona taasisi mpya ya KOTETI inainuka na kutimiza malengo makubwa mapya iliyopewa ya kuongeza ujuzi kwa watanzania kwa kozi ya ufamasia (Pharmacy)  na kozi mbalimbali zitakazo endelea kutolewa katika Chuo hicho cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) kinacho milikiwa na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Kwa upande wake Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi ya maendeleo anayoyafanya sana sana mradi wa kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ambao utasaidia katika upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuondoa tatizo la uhaba wa umeme nchini pamoja na kupunguza gharama za umeme kwa Watanzania.

Askofu Dkt. Mbilu ameipongeza serikali kwa juhudi walizozionyesha kupitia Waziri wa nishati Mhe. January Makamba/ Mbuge wa Bumbuli kwa ushirikiano waliouonyesha na kuwashika mkono katika mchakato wa kuanzisha Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI.) ambacho kwa sasa tayari kinatoa Kozi ya Ufamasia (Pharmacy) inayohusika na kuandaa, kuchanganya na kutoa dawa za kimatibabu kwenye mahospitali, maduka ya madawa, na viwandani.