Kristo anasema: "KILA ANIAMINIYE AJAPOKUFA ATAKUWA ANAISHI."

Askofu wa KKKT- Dayosisi ya Kaskazani Mashariki Mch. Dkt Msafiri Joseph Mbilu ,anasikitika kutangaza kifo cha Mch. Sabina Lumwe  kilichotokea leo tarehe 08/01/2023 nyumbani kwake Lushoto. Ibada ya mazishi itafanyika siku ya jumanne ya tarehe 10/01/2023 Kanisa Kuu  (cathedral) Lushoto na itaanza saa 4:00 asubuhi.

Marehemu Mch. Sabina Lumwe alikua ni mchungaji mstaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambapo alitumika katika Sharika na vituo mbalimbambali taarifa zaidi juu ya msiba huu zitaendelea kutolewa.

Uongozi wa KKKT-DKMs unatoa pole kwa familia ya Marehemu, wana KKKT-DKMs ndugu, jamaa na marafiki popote pale walipo. BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na lihimidiwe.

Mnamo tarehe 30/06/1991 historia iliandikwa KKKT-Dayosisi ya Kasakazini Mashariki ambapo wachungaji wanawake watatu walibarikiwa na kuingia katika huduma ya kichungaji marehemu Mch. Sabina Lumwe akiwa mmoja wao.

Marehemu Mchungaji Sabina Lumwe aliadhimisha miaka 30 tangu kubarikiwa kuwa mchungaji tarehe 15/08/2021 katika Ibada iliyofanyika Kanisa Kuu Lushoto. Mnamo mwaka 1979 KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilichukua uamuzi kupitia vyombo vyake vya maamuzi kupeleka mwanamke wa kwanza kwenda kusomea theolojia  katika Chuo cha Uchungaji Makumira. Jambo hili lilikua ni jambo jipya sio tuu kwa Dayosisi yetu bali pia kwa Kanisa zima la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Hii ni kutokana na mapokeo mbalimbali katika kila Dayosisi.

 Haikuwa jambo rahisi kutokana pia na mtazamo wa jamii ilivyokuwa inawachukulia wanawake kutumika katika huduma ya kichungaji ndipo mwaka 1981 Wanawake wengine wawili walipelekwa kujiunga na masono ya Theolojia. Baada ya kumaliza masomo walipangwa kwenye Sharika kutumika kama Watheolojia.  Hawakufanya mambo ya kichungaji kwa mfano; kutoa Chakula cha Bwana, kufungisha ndoa na ubatizo bali walihusika katika kuongoza Ibada zikiwemo Ibada za mazishi, kufundisha madarasa ya Kipaimara, kufundisha Elimu ya Kikristo mashuleni, kufundisha wainjilisti na mashemasi na kuongoza idara za akina mama.

Katika kipindi chote hicho mijadala mbalimbali ya kubariki wanawake kuwa wachungaji iliendelea katika Dayosisi na Kanisa kwa ujumla.  Mwaka 1990 Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania katika Mkutano wake Mkuu uliofanyika Morogoro pamoja na mambo mengine walifanya uamuzi wa  kubariki wanawake kuwa wachungaji. Ndipo uhuru ukatolewa kwa Dayosisi zile ambazo zilikuwa  tayari kufanya hivyo.

Mwaka 1991 Juni 30 muda mfupi baada ya uamuzi huo ndipo KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ilipoamua kuwabariki wanawake wa kwanza kuwa wachungaji. Ibada ya siku hiyo iliongozwa na Hayati Askofu Dkt. Sebastian Kolowa akishirikiana na Askofu Elinaza Sendoro wa KKKT-Dayosisi ya Mashariki na Pwani. Hata hivyo Halmashauri Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki iliwapa fursa wachungaji hawa wanawake ya kufanya kazi kwenye Sharika, Kurugenzi, Idara na Vituo ndani ya Dayosisi na katika KKKT kwa nyakati tofauti.