MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ameishauri serikali kushughulikia kwa ukali tuhuma za ubadhirifu zinazosikika kuiandama miradi mikubwa yenye manufaa kwa taifa. Askofu Dkt. Shoo pia amesema Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania haliungi mkono vitendo vya ushoga na ndoa za jinsia moja na halitoacha kutumia rangi za upinde wa mvua kwenye nembo yake kwa kuwa "ni agano la Mungu".



Askofu Dkt. Shoo, ameyasema hayo hapo jana tarehe 07/05/2023  kwenye Ibada ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini kwa Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Dodoma, Mch Christian Ndossa:- "Ninaipongeza serikali kwa miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa kwa sasa. "Tunaombea miradi isimamiwe vizuri na kukamilika kwa wakati na ikiwa hivyo, miradi itakuwa na manufaa makubwa kwa taifa hili na mataifa jirani.

"Jambo kubwa tunaloomba - shughulikieni kwa ukali sana tuhuma za ubadhirifu tunazozisikia zinazoanza kuandama miradi hii mikubwa na kwa manufaa ya taifa letu. Shughulikieni kwa ukali na kwa maneno," alisema