Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ametoa wito kwa wafanyabiashara, wadau mbalimbali wa elimu na maendeleo pamoja na Watanzania kwa ujumla kuungana na KKKT-DKMs kwenye harambee kubwa yenye lengo la kuchangia kazi za maendeleo na Vituo vya Diakonia vya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki itakayofanyika tarehe 18/08/2023 Jijini Dar Es Salaam.
Askofu Dkt. Msafiri Mbilu amesema kuwa pamoja na umuhimu mkubwa wa vituo hivyo, vinakabiliwa na ugumu katika uendeshaji wake kutokana na uchakavu wa miundo mbinu yenye umri wa zaidi ya miaka 100, uhaba mkubwa wa vifaa vya kutolea huduma na madeni makubwa.
Askofu Dkt. Mbilu ametoa witu huo leo tarehe 04/08/2023 wakati akiongea na waandishi wa habari jiji Dar es salaam na kueleza kuwa harambee hiyo kubwa itafanyika tarehe 18/08/2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye harambee hiyo ambapo fedha zitakazo patikana zitasaidia katika kuimarisha miundo mbinu ya vituo hivyo, kununua vitendea kazi vikiwemo vifaa tiba, pamoja na kupunguza madeni mbalimbali yanayovikabili vituo hivyo.
KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, ilianzishwa mwaka 1890, pamoja na kazi za Uinjilishaji imeendelea kutoa huduma za Kiroho na za Diakonia kwa watu wote wakiwemo wenye mahitaji maalum. Vituo hivyo ni kama vifuatavyo:- Irente Childrens Home, Irente School for the Blind, Rainbow School .
Lutindi Mental Hospital (Hospital ya kwanza ya Wagonjwa wa akili Afrika Mashariki), Bumbuli Hospital (hapa ndipo ilipoanzia Hospital ya KCMC ambayo baadae ilihamishiwa Moshi mwaka 1972), Hospital 3 na Dispensari 10 zilizoko chini ya Hospital ya Bumbuli, pamoja na Chuo cha Kolowa Technical Training Institute(KOTETI) kilichopo kwenye majengo ya kilipokuwa Chuo Kikuu cha SEKOMU kilichofungwa mwaka 2019.