MATUKIO KATIKA PICHA:- Ibada ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Arusha tarehe 21/08/2023.

Sehemu ya historia fupi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT) inaeleza kuwa:-

Historia ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania huanzia mwaka 1887, wakati Chama cha Misioni kutoka Ujerumani kilichojulikana kwa jina la Chama cha Misioni cha Berlin III au Evangelical Missionary Society for East Africa (EMS) kilipoanzisha kazi ya Injili Dar es Salaam. Huu ndio mwanzo wa Kanisa la Kilutheri Tanzania. Baada ya takriban miaka mitatu na nusu, chama cha pili, pia kutoka Ujerumani, kiliingia Tanzania kikitokea Afrika ya Kusini na kuanza kazi Nyanda za Juu Kusini mwaka 1891.  Chama hiki kilijulikana kwa jina la Chama cha Misioni cha Berlin I. Chama hiki kilianzisha kituo au misheni sehemu iitwayo Ipagika au Pipagika (Wangemannshöhe) katika Dayosisi ya Konde leo.

Mnano mwaka 1890 Chama cha Berlin III kilibadilika kufuatana na haja iliyokuwepo na kikachukua sura mpya baada ya kubadili sera yake na kujulikana kama Bethel au Misioni ya Bethel. Misioni hii ilifika Tanga na kuanza kazi mahali paitwapo Mbuyukenda. Kwa maneno mengine, kazi ya Berlin III ilihamishiwa kwa Misioni ya Bethel. Baadaye Misioni hii iliazimia kufikisha Injili ya Kristo nje ya mipaka ya Tanzania, wakaamua kwenda Rwanda. Ili kufika Rwanda, wamisionari walipaswa kupitia Bukoba. Walipofika Bukoba mwaka 1910 wakashawishika kufungua kituo Bukoba na ile nia ya kuanzisha kazi ya mission Rwanda ikawa imesitishwa.

Chama cha tatu kufika Tanzania kutoka Ujerumani kilijulikana kwa jina la Chama cha Misioni cha Leipzig. Chama hiki kiliingia nchini Tanzania mwaka 1893 na kuanza kazi ya mision Kaskazini mwa nchi sehemu ya Kitimbirihu, Old Moshi, kituo ambacho kilinunuliwa kutoka misioni ya Kianglikana – Church Missionary Society (CMS) mwaka wa 1892. Kwa kushauriwa na Carl Peters, mtawala wa kijerumani, wamisionari hawa waliendelea hadi Nkwarungo – Machame kuanzisha kituo chao cha kwanza. Vyama hivi vitatu ndivyo vilivyoeneza Ulutheri nchini Tanganyika

Tofauti na wamisionari wa vyama vingine, hawa wamisionari Walutheri waliotoka Ujerumani walikuwa na kanuni ya kujifunza lugha za wenyeji ambao walikusudia kuwapelekea Injili. Kwa maneno mengine, waliwahubiria na kuwafundisha wenyeji kwa lugha zao za asili ili Injili yake Kristo iwafikie katika lugha zao wenyewe.

Kutokana na vyama hivi vitatu vilivyoanzisha Ulutheri Tanzania, pamoja mchango wa vyama vingine vya misioni vilivyofuata kutoka Ulaya na Marekani (FELM, SEM, CoS, DLM, DANM, LMW, MEW, NLM, NMZ, UEM,VELKD, ELCA, BMW), Neno la Mungu limeendelea kuenezwa. Vituo vya elimu ya msingi, kati na sekondari, na vyuo vya ufundi na ualimu, zahanati na hospitali vilianzishwa kwa lengo la kumhudumia mwanadamu mzima – mwili, roho na akili. Kazi kubwa ya Kanisa la Kilutheri tangu lilipoanzishwa ni kueneza Ufalme wa Mungu kwa kufundisha na kuhubiri Injili ya Yesu Kristo kwa usahihi.

Kanisa la Kilutheri limeenea Tanzania na kuvuka mipaka yake kwa njia ya Missioni yake. Tangu 1963 makanisa saba yaliungana na kuanzisha Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Kanisa hili limeongezeka na kufikia dayosisi 27. Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba Kanisa hili la Kilutheri limedumu katika mafundisho sahihi ya Neno la Mungu.

Uzinduzi wa umoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ulifanyika kwa upendo mkubwa uliojaa imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa kuzingatia na kukumbuka kwamba ni mapenzi ya Bwana wa Kanisa kwamba watu wake wawe na umoja kama Yeye na Baba walivyo umoja, Yaliyokuwa makanisa saba (7) ya Kilutheri yaliamua kushirikiana na kuungana pamoja na kutokeza KKKT. Hayo makanisa saba yalikuwa kama ifuatavyo:

  • Kanisa la Kilutheri la Iraqw
  • Kanisa la Kiinjili la Tanganyika ya Kaskazini
  • Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya
  • Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya
  • Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya
  • Kanisa la Kilutheri la Uzaramo-Uluguru
  • Kanisa la Kilutheri la Usambara-Digo

Makanisa haya saba ya Kilutheri ambayo huko nyuma yalishirikiana kwa njia ya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Tanganyika tangu mwaka 1938, walianzisha Ukurusa mpya katika historia ya Kanisa la Kilutheri hapa nchini Tanganyika ambayo kwa sasa ni Tanzania. Umoja huu mpya wa kufanya kazi ya kueneza Injili ya Bwana Yesu ulifanywa kwa makubaliano ya hiari au muungano wa hiari kutoka kila Kanisa mwanachama.

Makanisa haya saba yaliyofanya kazi pamoja yakaweka tofauti zao za vyama anzilishi mbali na kuungana kwa kuzikubali kanuni na sheria walizojiwekea kuwa maongozi ya maisha ya umoja wao katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanganyika sasa Tanzania. Umoja huo ulianza tarehe 19/6/1963.

  1. Yoram Girgis na Finn Espegren kuwakilisha Kanisa la Kilutheri la Iraqw.
  2. Stefano Moshi na M.A. Shaidi waliowakilisha Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kaskazini.
  3. Matia Lutosha na Bengt Sundkler waliowakilisha Kanisa la Kiinjili la Tanganyika ya Kaskazini
  4. Thomas Musa na Manase Yona waliowakilisha Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kati.
  5. Lunogelo Vuhahula na A.M. Kalyoto waliowakilisha Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kusini.
  6. Daniel E.K. Magogo na Elirehema Philipo Mwanga waliowakilisha Kanisa la Kilutheri la Usambara-Digo (Ambaye hata sasa bado yuko hai) na 
  7. Von Sicard na Immanuel Barnabas waliowakilisha Kanisa la Kilutheri la Uzaramo- Uluguru.

Waasisi hawa wa KKKT (ELCT) waliweka wazi Msingi wa Imani utakaofuatwa na KKKT kama ifuatavyo (kwa tafsiri isiyo rasmi)

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanganyika (Tanzania) lililojengwa juu ya msingi mmoja, Yesu Kristo, hukiri kwamba Neno la Mungu lililoandikwa katika Agano la Kale na Agano Jipya ndio msingi pekee wa uhakika wa Imani na maisha ya Kanisa. Katika Umoja wa Kanisa moja duniani, huungama Ungamo la Mitume na la Nikea na la Athanasio; hukubali pia maungamo ya Kanisa la Kilutheri hasa Ungamo la Augsburg lisilobadilishwa na Katekismo Ndogo ya Martin Luther kuwa ni maelezo au mafafanuzi sahihi ya Neno la Mungu. Sharika zote, na wachungaji, Sinodi na Dayosisi za Kanisa hili zitakubali na kufuata msingi huu wa Imani.

Tangu mwaka 1963 makanisa saba yaliyoanzisha KKKT yamedumu katika umoja na ushirikiano na idadi ya Wakristo Walutheri nayo ikizidi kuongezeka. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba kutoka kazi iliyoanzishwa mwaka 1887 hadi kufikia maadhimisho haya ya miaka 60 ya KKKT, idadi ya dayosisi imeongezeka na kufikia 27. KKKT pia imefanya kazi ya misioni ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, hasa katika nchi Jirani ambazo ni Kenya, Msumbiji, Zambia, Malawi Kongo (DRC), Burundi, Rwanda na Uganda. Tangu kuanza kwa KKKT, kazi kubwa ya kueneza Injili na kuanzisha makanisa mapya imefanywa na wakristo wa kawaida waliokuwa watumishi wa serikali au wafanyabiashara. KKKT inawashukuru watumishi hao waliotimiza wajibu wao kwa vitendo kwa kumheshimu na kumtii Bwana wao Yesu Kristo ambaye aliagiza kwamba “Endeni mkawafanya mataifa yote kuwa wanafunzi...” (Mt.28:19-20)

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania huonekana pia kung’ara katika uimbaji ndani ya ibada na pia katika wingi wa kwaya mbalimbali katika sharika na mitaa yake. Uimbaji kama sehemu ya ibada hufuata utaratibu na uchaji wa ibada. Sifa na shukrani ni kwa Mungu aliyeotesha punje ndogo ya haradali hadi kufikia kilele hiki cha kusherekea miaka sitini ya KKKT. Kanisa linaendelea kuwahimiza washarika wake kuendelea kutimiza wajibu wao kwa Bwana wao Yesu   Kristo. Kwa kuzingatia tunu za Kanisa, washarika wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika huduma zinazotolewa na Kanisa, huduma hizo ni Ibada ya neno na Sakramenti, elimu, afya, udiakonia, na huduma za kiuchumi. Kanisa litaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha kwamba binadamu anahudumiwa kwa ukamilifu katika mahitaji kwa utaratibu kwa; Kuwapa nafasi/kuwahusisha makundi maalumu katika huduma mbalimbali za Kanisa, kusimamia misingi ya Imani ya Kikristo na mafundisho ya kweli ya Neno la, kuchangia katika kukuza na kuinua maendeleo ya nchi na Bwana wa Kanisa, ataendelea kulitunza Kanisa lake hadi atakaporudi yeye mwenyewe. Neema na iwe na kila msharika wa KKKT.