Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Michael Mlondakweli Kanju amewaasa Washarika wa Kabuku, Jimbo teule la Magharibi na Wakristo kwa ujumla kuchora alama ya msalaba mioyoni mwao na kumkaribisha Yesu katika maisha yao na waache kuangalia ukubwa wa tatizo na badala yake wamwangalie Yesu. Pia amesema wakianguka na kushindwa wasizame kwenye dhambi bali waamke na kuutafuta uso wa Bwana.
Sambamba na hayo amewashukuru wana KKKT-Dayosisi ya Kaskazini kwa kuendelea kuwaombea pamoja na mshikamano wanao uonyesha katika kipindi hiki kigumu cha madeni yanayo ikabili Dayosisi. Ameongeza kuwa Kanisa ni chombo cha kutenda haki na hakuna mtu ambaye haki yake itadhulumiwa na madeni yameanza kulipwa kutokana na michango inayoendelea kutolewa na wana Dayosisi pamoja na wadau wengine wa maendeleo. Ameyasema hayo katika Ibada ya Kipaimara iliyofanyika Jimbo Teule la Magharibi ,Usharika wa Kabuku tarehe 17/09/2023
Katika Ibaada hiyo Msaidizi wa Askofu Mch. Kanju alimbatana na Mkuu wa Jimbo Mteule wa Jimbo Teule la Magharibi Mch. Ismael Ngoda na Mch. kiongozi wa Usharika wa Kabuku Mch. Paulo Kivatiro.
Jumla ya Vijana wakipaimara 106 wamebarikiwa na watatu kati yao walibatizwa, huku wakiunga mkono juhudi anazozifanya Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu katika kukabiliana na deni la Dayosisi kwa kuchangia kiasi cha Tsh. 318,000/= huku wakiungwa mkono na wazazi pamoja na Washarika waliohudhuria katika Ibada hiyo na kufanya jumla kuu ya mchango wao kuwa Tsh 891,950/=