Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch. Michael Mlondakweli Kanju amewataka Washarika wa Usharika wa Mkata na wakristo kwa ujumla kumuamini Mungu na kumpa nafasi katika maisha yao pindi wanapokutana na changamoto mbalimbali katika maisha, na kuacha tabia iliyozuka katika jamii ya kujitoa uhai.

Hayo ameyasema tarehe 30/09/2023 alipokua akihubiri katika Ibada iliyofanyika katika usharika wa Mkata Jimbo Teule la Magharibi ambapo Ibada hiyo ilikuwa na tendo la kuwabariki vijana wa Kipaimara pamoja na ubatizo.

Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju amesema wapo watu wengi wanaokutana na changamoto mbalimbali katika maisha na wengine hata kuchukua uamuzi wa kujiua jambo ambalo halimpendezi Mungu hivyo kuwataka Wakristo wamkimbilie Mungu pindi wanapokutana na mambo magumu, kwani Mungu ameahidi kushuhulika na maisha ya walewote wanao mwamini na kumtumikia,kwani hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani uzima wa milele. Katika Ibada hiyo jumla ya Vijana wa Kipaimara wapatao 29 wamebarikiwa na mmoja kati yao alibatizwa

Katika Risala ya vijana hao waliobarikiwa iliyosomwa mbele ya msaidizi wa Askofu Mch. Michael Kanju vijana hao wamempongeza Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu  kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha Dayosisi inapiga hatua mbele.Wameongeza kuwa kwa hakika wanajivunia uongozi wa Baba Askofu kwa uchapakazi na uongozi wake makini,  kasi ya tofauti katika kuleta maendeleo katika Dayosisi hivyo kuungana na uongozi kwa kutoa kiasi cha Tsh. 174,000 kwaajili ya kuchangia deni la Dayosisi, ambapo mara baada ya kuungwa mkono na wazazi, walezi pamoja na watu mbalimbali walioshiriki katika Ibada hiyo jumla ya kiasi cha Tsh.847, 900 kilikusanywa na kuelekezwa katika ulipaji wa  deni la Dayosisi.

Vijana hao wameitumia siku hii muhimu kwao kumshukuru  Mungu aliyewalinda na kuwatunza  tangu  walipoanza mafundisho  hadi leo hii wanapobarikiwa kwani safari ya miaka miwili haikuwa nyepesi, lakini Mungu amewawezesha.

Wamekiri  kufundishwa vizuri Neno la Mungu kwa usahihi na kufahamu kuwa wokovu wao ni katika Kristo Yesu wala si katika mwingine. wamejifunza Imani ya Kikristo vizuri, sakrament, uwakili  na kuishi maisha ya Kikristo. Kwa msingi huo wameahidi  kutoyumbishwa na mafundisho potofu ambayo yameenea kote duniani.

Vilevile  vijana hao waliobarikiwa wameshukuru kwa malezi mema ya kiroho waliyopokea kwa walimu, Wainjilist na Mchungaji. Aidha wamewashukuru wazazi kwa kuwalea na kuwahimiza kwenda kanisani na kwenye mafundisho.

Mwisho wamemshukuru kipekee Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu  kwa kufikia siku hii muhimu inayoweka alama katika maisha yao kwani kufika kwao siku ya leo kumechangiwa na  uongozi shupavu wa Baba Askofu kwani moja ya vipaumbele vyake ni mafundisho sahihi na hayo wameyapata na wataendelea kuyapata.