Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki amewashukuru washarika wa Usharika wa Tamota na wanadayosisi kwa ujumla kwa namna wanavyoendelea kushikamana na kujitoa katika kumtumikia Mungu.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa shukrani hizo tarehe 29/10/2023 kwenye Ibada iliyokuwa na tendo  la kuwabariki vijana wa Kipaimara pamoja na uwekwaji wa jiwe la Msingi la Kanisa katika Usharika huo na kuongeza kuwa mshikamano uliopo utawezesha kukamilika kwa ujenzi unaoendelea wa Kanisa hilo.

 Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu amewashukuru wanadayosisi kwa namna wanavyojitoa kwa michango yao kwa kuchangia deni la Dayosisi, na kusisitiza kuwa pamoja na uwepo wa deni linaloikabili Dayosisi bado  kazi za maendeleo zimeendelea kufanyika nazitaendelea kufanyika.

Wakisoma Risala kwa Baba Askofu Vijana hao wameeleza mafanikio waliyoyapata kutoka kwa walimu wao kwa kipindi cha miaka miwili kwenye darasa lao la Kipaimara.

Wameeleza kuwa wameandaliwa vizuri kiimani ili waweze kua mashahidi wema na waaminifu wa Kristo na kuweka ahadi ya kusimama katika Imani ya Kikristo. Pamoja na mambo yahusuyo Imani vijana hao wamekiri kufundishwa na kuhimizwa juu ya Elimu kwa ajili ya ustawi wa maisha yao ya baadae kwa kusoma kwa bidii ili waweze kuyafikia malengo yao huku wakimtanguliza Mungu katika maisha yao.

Aidha vijana hao waliobarikiwa wapatao 80 na kati yao mmoja aliyebatizwa wamempongeza Baba Askofu kwa utumishi wake na kumuunga mkono kwa kutoa kiasi cha Tsh 495,000 kwa ajili ya kuunga juhudi za kuinua kwa upya vituo vya Dayosisi, ambapo vijana hao waliomba kuungwa mkono na wazazi pamoja na walezi wao na kufanya kiasi kilichokusanywa kufikia 700,300.

Hits: 2216