Print

Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu tarehe 01/11/2023 ameongoza  Ibada ya mazishi ya marehemu Mch. Msataafu Mzee Mpewa Lazaro Ruwa iliyofanyika katika Jimbo la Pwani Usharika wa Makorora Tanga.

Marehemu Mzee Ruwa aliitwa mbinguni tarehe 28/10/2023  akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo na mwili wake umepumzishwa tarehe 01/11/2023 katika makaburi yaliyopo katika eneo la Gofu Tanga.

Marehemu Mzee Ruwa amefariki akiwa na umri wa miaka 86, ameacha watoto 7, wakike 5 na wakiume 2, wajukuu 7, wakike 4 na wakiume 3 na kitukuu 1.Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki unaendelea kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu.

 KUZALIWA:-Marehemu alizaliwa mwaka 1937 katika kijij cha Vunde Gombero Wilayani Mkinga mkoani Tanga wazazi wake wakiwa ni Hayati Lazaro Ruwa na mkewe Bi: Anna Sitti akiwa ni miongoni mwa watoto Alibatizwa na kupata kipaimara katika Kanisa la KKKT Gombero Tanga

 MASOMO NA ELIMU:-Marehemu alipata elimu yake ya Msingi mwaka 1942-1950 katika shule ya msingi TABORA GOMBERO na baadae mwaka 1951 shule ya msingi Mkinga. Aliendelea na masomo ya kati katika shule ya Sekondari ya Old Tanga kuanzia mwaka 1952-1955, ambapo alihitimu darasa la 8.

 KUAJIRIWA:-Marehemu aliajiriwa kama KARANI katika vipindi tofauti vifuatavyo:-Karani Mamlaka ya Bandari Tanga- 1956-Karani Shamba la mkonge Mjesani Estate kwa muda mfupi mwanzoni mwa mwaka 1960.Karani wa KODI katika mwaka 1960 hadi mwishoni alipopata wito katika mwaka 1961 kuanza kazi za kanisa

KUANZA MASOMO YA KAZI ZA KANISA

  1. Mwaka 1961-1962 alianza masomo katika shule ya Biblia Mwika – mkoani Kilimanjaro
  2. Mwaka 1963-1967 alichukua masomo ya Theologia katika chuo cha uchungaji kilichoko Makumira- Mkoani Arusha
  3. Mwaka 1966 alifanya mazoezi katika shule ya Biblia Mwika na mnamo mwaka 1967 alirudi tena kumalizia masomo yake ya Theologia katika ngazi ya cheti Makumira.
  4. Mwaka 1968 alibarikiwa kuwa Mchungaji na mwaka huohuo alitumwa kwenda kuwa Mwalimu katika shule ya Biblia Mwika hadi 1970

KUANZISHA KAZI YA USHARIKA MAKORORA TANGA

Mnamo mwaka 1971 alitumwa kuanzisha kazi ya Usharika wa Makorora Tanga ambao ulikuwa ni miongoni mwa Mitaa ya Usharika wa Kana Tanga, alitumikia Usharika wa Makorora kwa kipindi cha miaka 18, ikiwa wakati huo ni Usharika uliohudumia maeneo ya Misioni hadi mpakani mwa nchi jirani ya Kenya eneo la Duga Maforoni, vilevile itakumbukwa ya kwamba akiwa katika utumishi huo akishirikiana na Baraza la Wazee wa Usharika walianzisha Mtaa wa Mikanjuni ukiwa ni miongoni mwa mitaa ya Usharika wa Makorora ambao kwa sasa ni Usharika kamili.Mnamo mwaka mwaka 1989 aliitwa kutumikia Usharika wa Maramba Tanga, ambao alihudumu hadi mwaka 1998 alipostaafu kwa mujibu wa utumishi. Aliendelea kuishi Maramba na kujishughulisha na utumishi pamoja na kilimo kwa amani na furaha kubwa. Pia katika utumishi wake aliwahi kuwa Mkuu wa Jimbo la Pwani kwa vipindi viwili mfulilizo. Marehemu alifunga ndoa takatifu na Bi: Lucy Tawi Emanuel Vesso mnamo mwaka 1973 katika Usharika wa Kana na kujaliwa kupata watoto 7 wa kike 5 na wa kiume 2.

Hits: 2325