Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ameongoza Ibada ya Jumapili ya tarehe 19/11/2023 katika Jimbo la Kusini, Usharika wa Ngulwi B ambapo kulikua na tendo la Kipaimara ambapo vijana wapatao 108 walibarikiwa na watatu kati yao kubatizwa.
Askofu Dkt. Mbilu amewaasa na kuwakumbusha Washarika wa Ngulwi B na Wakristo wote kwa ujumla kuwa “Hukumu ya Bwana inakuja na kujiandaa na uzima wa ulimwengu mpya, na ujumbe huu umekuja pale ambapo Kanisa linaelekea mwisho wa mwaka na kuelekea katika mwaka mpya wa Kanisa (Adventi)”.
Sambamba na hayo, Baba Askofu Dkt. Mbilu amewashukuru washarika wa Ngulwi B ambao wapo ndani ya Jimbo la Kusini ambalo ndio linaloongoza katika kuchangia deni la Dayasisi kwa awamu hii ya tatu na kuwapongeza Washarika wote wa KKKT-DKMs kwa kuendelea kuchangia deni la Dayosisi.
Deni hili deni la kurithi lilikua kiasi cha shilingi 7,550,999,122/=(Bilioni saba milioni mia tano hamsini laki tisa tisini na tisa elfu mia moja ishirini na mbili) na kulifanya kupungua kwa kiasi kikbwa na kulifanya deni hilo kuwa Tsh 5,973,691,589/=(Bilioni tano milioni mia tisa sabini na tatu laki sita sitini na moja elfu mia tano themanini na tisa) na ametoa wito kwa wale ambao hawajamaliza michango yao ya shilingi elfu 30000 mpaka kufikia kilele chake tarehe 17/12/2023 kitakachofanyika Jimbo la Tambarare Korogwe kumaliza ahadi hiyo.
Katika kuelekea kwenye sikukuu za Krismasi,Askofu Dkt Mbilu amezitaka kwaya zote kuanza mazoezi ya wimbo wa Krismasi ambao ni wimbo namba 9 utakaoimbwa na kwaya zote za KKKT-DKMs na pia amewashauri wa tunzi wa nyimbo kutotunga nyimbo kwa kutumia ala za muziki kwasababu kupitia njia hiyo inaleta changamoto ya kutokua na uhuru wa kuwa na noteni (Noten) nyingi kwenye wimbo.
Vijana wa kipaimara wakisoma Risala yao kwa Askofu Dkt. Mbilu, wamempongeza kwajinsi anavyoendelea kupambana usiku na mchana katika kulipa deni la Dayosisi na hivyo waliunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia kiasi cha Tsh 324,000/= na baadaye kuungwa mkono na wazazi na walezi na jumla kuu kuwa Tsh 752,650/=
Aidha baada ya Ibada, Askofu Dkt. Mbilu alipata wasaa wa kwenda katika Mtaa wa Shembekeza kumtembelea Bi. Christina Sheshangali ambaye alikua mwanafunzi wa Chuo cha Biblia Vuga na kwa kutokana na ajali mbaya aliyoipata mwaka 2008 iliyomsababishia matatizo kwenye uti wa mgongo alishindwa kuendelea na masomo yake ya Uinjilisti.
Naye,Mwinjilisti Apelesi Sheshangali ambaye ni Baba mzazi wa Christina ametoa shukrani za dhati kwa Baba Askofu Dkt Mbilu na uongozi wa Dayosisi kwa ujumla, kwa kuendelea kumtunza binti yake ambaye hapo nyuma alikua amesahaulika kabisa, hii imepelekea faraja sana kwa Christina kwani inamuwezesha kupata tiba kwa wakati na uangalizi mkubwa.