Askofu wa KKKT -Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, Tarehe 24 / 11 / 2023 ameanza ziara yake ya Kikazi Katika Jimbo la Tambarare Usharika wa Mtonga na kuongoza Ibada zilizokuwa na matendo mbalimbali ikiwemo uwekaji wa jiwe la ufungizi wa Kanisa Mtaa wa Ngua,Ibada ya kuweka jiwe la msingi la Kanisa Mtaa wa Tabora, Ibada ya kuwabariki Vijana wa Kipaimara katika Mtaa wa Sayuni na ufunguzi wa Kongamano la ITA NAE ATAITIKA linalofanyika katika Senta ya Usharika wa Mtonga.
Akiwa katika uzinduzi wa Kongamano la maombi na maombezi la ITA NAE ATAITIKA Askofu Dkt. Mbilu ameipongeza Kurungezi ya Misioni na Uinjilisti ya KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kwa kuendelea kubuni njia mbalimbali za kueneza Neno la Mungu na watu kuijua kweli ya Kristo kupitia kituo Cha Radio Cha Utume FM kinachomilikiwa na KKKT-DKMs.
Askofu Dkt.Mbilu pia ametoka wito kwa Wakristo kumuita Mungu kilawakati katika maisha yao na kujihadhari na Mafundisho potofu ya neno la Mungu na kuzikataa sauti za Manabii na mitume wa uwongo wanaopotosha kweli ya neno la Mungu kwa maslahi yao binafsi.
KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kupitia kituo chake cha Redio Utume kwa miaka minne kupitia Idara ya Vipindi ilianzisha kipindi cha maombi kwa njia ya simu ‘Prayer Line’ siku za Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia majira ya saa 9:30 Alasiri hadi 11:00 Jioni kwa lengo la kuwahudumia wasikilizaji wenye uhitaji wa usaidizi wa huduma ya Kichungaji ambao kwa wakati huo walikuwa wakihitaji usaidizi wa kichungaji na kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kuwafikia.
Baada ya kipindi kuanza kurushwa hewani ilionekana kuwa bado kunauhitaji zaidi wa kufanyika maombezi kwa njia ya redio hivyo kikaanzishwa kipindi pacha cha “Ita nae Ataitika” kila siku za Jumapili kuanzia majira ya saa 4:00 usiku hadi saa 10:30 alfajiri.
Kupitia vipindi hivyo, kituo kilipata maono ya kuendesha Kongamano la Maombi na Maombezi na Ushauri wa Kiroho ambayo pia yalilenga kuingiza fedha kupitia sadaka, kuuza bidhaa nyingine za redio kama matangazo madogomadogo, kadi za salamu na Tshirt fedha zilizolenga kusaidia gharama za uendeshaji wa kituo.
Hadi sasa redio imeandaa na kufanya makongamano matano ya maombi na maombezi, matamasha mawili yamefanyika Wilayani Lushoto KKKT-DKMs Usharika wa Kanisa Kuu (Cathedral) Lushoto, tamasha moja KKKT-DKMs usharika wa Mombo, KKKT-DKMs Usharika wa Gombero Senta Kwediboma Kilindi na KKKT-DKMs Usharika Mteule wa Misima Handeni.
Malengo ya Kongamano,Kufikisha Injili sahihi ya Yesu Kristo kwa watu wote ili waokolewe. Malengo Mahususi: Kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya redio ‘TUNAKUFIKIA HAPO ULIPO’ Kuifanya Redio Utume kuwa chombo cha habari kinachosikilizwa zaidi katika Mkoa wa Tanga.