Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amesema katika uongozi wake ataendelea kutambua mchango na kazi kubwa iliyofanywa na Wachungaji, Mashemasi pamoja na watumishi wengine waliostaafu ambao walioitumikia Dayosisi kwa nyakati tofauti na kuongeza kuwa pamoja na kustaafu utumishi wao bado wanao mchango wa uzoefu , ujuzi na uwezo wa kushauri ili kuondoa makosa katika utendaji.
Askofu Dkt. Msafiri Mbilu ameyasema hayo tarehe 28.11.2023 kwenye ufunguzi wa kikao chake na Wachungaji pamoja na Mashemasi Wastaafu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin William Mkapa Auditorium, uliopo katika, Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) Magamba Lushoto Tanga ambacho kitafanyika kwa siku mbili ambapo kitahitimishwa tarehe 29.11.2023.
Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu ameweka wazi kuwa wastaafu hao watapewa taarifa kutoka Kurugenzi ya Misioni na Uinjilisti,Kurugenzi ya Huduma za Jamii, Kurugenzi ya Uchumi na Mipango pamoja na Kurugenzi ya Fedha na Utawala ili wastaafu hao wapate nafasi ya kutoa maoni na ushauri wao.
Kwa upande wao Mch. Mstaafu Nkhanileka Chedi, Mch. Mstaafu Zawadiel Mkilindi pamoja na Mch. Mstaafu Yohana Mmaka wamesema wamefurahi kwa kupata nafasi ya kukumbukwa na Baba Askofu Dkt.Mbilu kama wastaafu nakuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuitumikia Dayosisi pamoja na kushauri juu ya mambo mbalimbali yanayohusu Dayosisi.
Kikao hicho kitaangazia kazi za maendelo ikiwemo miradi mbalimbali inayotekelezwa na Dayosisi pamoja na kuwasilishwa kwa taarifa ya maendeleo ya Shamba la Irente Farm, Taasisi ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) na Ujenzi wa vibanda vya biashara unaoendelea ndani ya Dayosisi.