Sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu, watumishi tulioitumikia KKKT- Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu Mwenyezi kwa jinsi anavyoendelea kututunza na kutubariki katika maisha yetu.Tunaamini kwamba katika historia imekuwa jambo la kipekee kuweza kukutana na kukaa kwa faragha pamoja na uongozi mzima wa Dayosisi yetu. Kwa hakika imekuwa nafasi muhimu lakini adhimu.
Tunayo kumbukumbu kwamba uongozi uliopo madarakani kwa sasa uliingia madarakani kuiongoza Dayosisi yetu katika kipindi kigumu sana, hasa tukizingatia mambo kadhaa ya msingi:
1.Ni kipindi ambacho Dayosisi ilikuwa imegawanyika sana
2.Waumini wa Dayosisi hii, walikuwa katika hali ya kukata tamaa kiasi cha baadhi yao kuwa wameihama Dayosisi yetu.
3.Sharika zetu na Dayosisi yetu kuonekana kutokuwa na mwelekeo thabiti.
4.Wachungaji, Mashemasi na waumini kugawanyika na hivyo kutoaminiana.
Hali hii imeufanya uongozi mpya wa Dayosisi uliopo madarakani kuwa na kazi ngumu ya mahali pa kuanzia, ingawa tunamshukuru Mungu kwa Neema yake kwa kuupa uongozi mpya Neema ya kuyaona hayo na kuamua kuanza kuchukua hatua nzuri na madhubuti kuiweka Dayosisi yetu katika mstari kwa kutengeneza na kujenga mwelekeo mpya. Miongoni mwa mambo muhimu tuliyoona yakifanyika ni pamoja na:
- Kurudisha mioyo ya waumini waliokata tamaa na mambo ya kiimani
2.Kuona namna ya kurudisha kwa upya uhusiano katika kuaminiwa na Serikali na marafiki zetu.
3.Uongozi wa kujiamini na kujenga moyo wa utayari katika kujitoa kutumika na sio kutumikiwa.
Tumeshuhudia kwa wazi jinsi mwelekeo huo mpya ulivyowekwa wazi katika kutumika kwa nguvu zote na kujenga upya Imani ya waumini na marafiki. Miongoni mwa mambo tuliyoshuhudia ni pamoja na:
- Uendelezaji wa miradi ikiwa ni kwa ajili ya kuifanya Dayosisi ilenge kujitegemea katika kipindi kijacho. Tunaona miradi ya vibanda vya biashara, kilimo, na kadhalika.
Kazi hizi zinazofanyika na nyingine nyingi zinazotazamiwa zinachagiza mchango mkubwa kwa maendeleo ya haraka ya Dayosisi yetu kurudi katika mstari kwa upya. Imani yetu ni kwamba, mambo haya yatairudisha Dayosisi yetu mahali pake.
Kwa ajili hiyo sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu, tuliokutana hapa KOTETI tarehe 28 hadi 29 Novemba, katika mwaka wa Bwana wetu, tunatumia nafasi hii kuupongeza uongozi Mpya wa Dayosisi yetu, kwa kipekee kinara mapambano ambaye ni Mheshimiwa Baba Askofu Dr. Msafiri Joseph Mbilu. Sisi Wachungaji na Mashemasi Wastaafu tunaweka ahadi kwake kwamba tutaendelea kumwombea afya njema na kumsaidia. Aidha tunamwambia kwamba kustaafu sio kuacha utumishi ila kustaafu ni kuwa uwanja mpya wa mapambano ya kiutumishi.
Ni sisi Wachungaji na Mashemasi wastaafu
Tumeitoa leo tarehe 29 Novemba, 2023.