Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu amewashukuru na kuwapongeza wanadayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa kujitoa kikamilifu katika kuchangia fedha kwaajili ya kulipa deni la Dayosisi, ambapo amewasihi kuongeza jitihada katika kuchangia deni hilo ili liweze kuisha na Dayosisi kuendelea kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo kwenye Ibada ya Jumapili tarehe 17/12/2023 iliyofanyika katika Usharika wa Korogwe ambapo Ibada hiyo iliambatana na kilele cha harambee ya uchangiaji wa Deni la Dayosisi kwa mwaka 2023 awamu ya Tatu.
Sambamba na hayo Askofu Dkt. Mbilu,ameongeza kwa kusema kuwa pamoja na deni kubwa linaloikabili Dayosisi lakini bado mambo mbalimbali ya maendeleo yameendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa vibanda vya biashara, mradi wa shamba la parachichi pamoja na Chuo cha Kolowa Technical Training Insitute (KOTETI) ambacho kwa sasa kina sifa ya kutoa kozi mbalimbali.
Askofu Dkt. Mbilu ameongeza kwa kusema kuwa awali Chuo cha KOTETI kilikua kinatoa kozi moja ya Ufamasia (Pharmacy), lakini baada ya serikali kuridhishwa na mwenendo mzuri wa Chuo kwa sasa Chuo kimepewa ithibati kamili kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) ambapo sasa Chuo kinaweza kudahili wanafunzi kwa kozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kozi ya Sheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha na Utawala CPA. Peter John Singano amemshukuru Askofu Dkt. Mbilu kwa jitihada zake nyingi na kwa kubuni njia mbalimbali za kuivusha Dayosisi katika kipindi hiki kigumu cha madeni huku akiwashukuru Washarika na Wadau mbalimbali wamaendelo wanaojitoa katika kuchangia Deni hilo.
Katika Ibada hiyo kiaisi cha Tsh.20,962,100 kilikusanywa, ahadi ilikuwa Tsh.676,000 na kufanya jumla Kuu kuwa Tsh.21,638,100.