Msaidizi wa Askofu, KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Dean Michael Mlondakweli Kanju amewashukuru Washarika wa Usharika wa Soni Mtaa wa Kwang’wenda kwa namna wanavyoendelea kujitoa kwa hali na mali katika kumtumikia Mungu sambamba na uchangiaji wa deni linaloikabili Dayosisi.
Dean Kanju ameyasema hayo wakati akihubiri katika Ibada ya Jumapili tarehe 04/02/2024 iliyofanyika katika Usharika wa Soni Mtaa wa Kwang’wenda iliyoambatana na tendo la Shukrani kwa familia ya Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, kwa mema mengi Mungu aliyowatendea.
Sambamba na hayo Dean Kanju amewataka Wana Dayosisi kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliopo katika kulikabiri deni la Dayosisi kwani litakwisha na kuziacha mali za Dayosisi zikiwa salama, huku akiwataka Wanadayosisi na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao tayari wameingia kazini na kuonesha moyo wa kuchangia deni hilo kuendelea kufanya hivyo pasipo kuyumbishwa.
Dean Kanju ameongeza kuwa ni wakati sahihi wa kumtia moyo mbeba maono wa Dayosisi Baba Askofu Dkt. Mbilu pamoja na uongozi wake katika kipindi hiki ambacho mipago na mikakati ya kulimaliza Deni la Dayosisi imeanza.
Katika hatua nyingine Dean Kanju amewataka wana Dayosisi kuwapuuza baadhi ya watu ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakiitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kueneza na kusambaza taarifa za uongo kuwa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki haidaiwi.
“Ni jambo la kushangaza kuona hao wanaosambaza habari za uongo kuwa Dayosisi haidaiwi lakini tayari watu hao wamepeleka malalamiko katika mifuko ya kijamii wakidai kulipwa stahiki zao ambazo zilishindwa kulipwa na uongozi uliopita Alisema Dean Kanju”.
Kwa upande wake Askofu Dkt. Msafiri Mbilu, ametoa wito kwa wana KKKT-DKMs na Wakristo kwa ujumla kutenga muda wa kumshukuru Mungu kwa mema mengi ambayo anawatendea katika maisha yao huku akiwashukuru wanadayosisi kwa namna walivyojitoa katika kuchangia deni la Dayosisi katika miaka iliyopita na kuwataka kuingia kwa nguvu mpya katika mwaka huu kuchangia deni hilo ili kunusuru mali za Dayosisi zisiuzwe.
Ameongeza kuwa Dayosisi ni kweli inadaiwa na kwakua Kanisa ni chombo cha kutenda haki wale wote wanaoidai Dayosisi watalipwa stahiki zao huku akiwasihi kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu kwani hakuna haki ya mtu itakayopotea