Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Mch Dkt Msafiri Joseph Mbilu, amewataka Vijana wa UKWATA Mkoa wa Tanga, kukubali kulelewa kiroho na kuwa mfano wa kuigwa wawapo shuleni kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo  kwa kufuata maadili mema na kuwa mstari wa mbele katika ufaulu mzuri darasani.

Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo tarehe 29/03/2024 kwenye ufunguzi wa kongamano la 59 la Ushirika  wa Kikristo wa Wanafunzi wa Tanzania (UKWATA) Mkoa wa Tanga unaofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin Mkapa uliopo  katika Chuo cha Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) Magamba Lushoto Tanga.

Ameongeza kuwa Kanisa linawajibu  wa kuwekeza  na kuweka nguvu ya ziada katika kuwalea Vijana ikiwa ni pamoja na kuwajengea msingi wa kuwa na maadili mema pamoja na kumjua Mungu kwani kwa kufanya hayo itawasadia Vijana kuondokana na mambo yasiompendeza Mungu katika Kanisa na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Tanga Kanisa la Anglikana CAN. Christopher Kiango ambaye amemuwakilishi Mwenyekiti wa CCT ambaye pia ni Askofu  Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Dkt. Maiombo Mndolwa,  amewaasa amewataka Walimu  kutofumbia macho baadhi ya Wanafunzi wanaofanya mambo  ambayo yanapelekea kuporomoka kwa maadili huku akiwataka  kutumia nafasi yao kama walezi kuwarekebisha tabia na mienendo yao. Amesisitiza Shule zinazomilikiwa na Kanisa ziwe mstari wa mbele katika malezi ya maadili mema na taaluma pia.

Kwa upande wa Vijana wa UKWATA Mkoa wa Tanga wameunga mkono juhudi za Askofu wa KKKT-DKMs Dkt Msafiri Joseph Mbilu katika kuchangia kazi za maendeleo katika Dayosisi  kwa kila mwana UKWATA  kuchangia kiasi cha shilingi 1,000 na wameahidi kushiriki katika kuiletea  maendeleo  Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kama Washarika wengine wanavyofanya.

Jumla ya vijana 600 wanashiriki kongamano la Pasaka Magamba Lushoto wakiongozwa na Neno kuu la Kongamano hiloi kutoka Mithali 23:26 "MWANANGU NIPE MOYO WAKO". Pia mada zitakazojadiliwa katika Kongamano hilo ni “Kijana Mkristo na Utandawazi” ,“Kijana Mkristo na Ujasiliamali” ambalo litafundishwa na muwezeshaji kutoka YOUTH PEACE MAKER Ndg. Peter Jali ,“Maadili kwa vijana” ambapo litafundishwa na Mwl Shengovi,”Habari za Ukombozi “ litafundishwa na Ndg. Vuriva na mada ya mwisho itakua ni “Urafiki,Uchumba hadi Ndoa”.