Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, anaendela na ziara yake ya kikazi iliyoanza tarehe 26/04/2024 nchini Marekani katika Mji wa Philadelphia, ambako ndiko Makao Makuu ya Synod rafiki ya Southeastern Pennsylvania yalipo. Hii ni mojawapo ya Synod za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Marekani.

Askofu Dkt. Mbilu ambaye ameambatana na msaidizi wake Dean Michael Kanju wapo nchini Marekeni kufuatia mualiko wa Askofu Dkt. Patricia Davenport Mkuu wa Synod hiyo yenye urafiki na KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki  kwa miaka zaidi ya 30 sasa.

Pamoja na mambo mengine  ziara hii ina lengo la kuimarisha uhusiano uliopo ikiwa ni pamoja na kushiriki Mkutano Mkuu wa Synod hiyo utakao fanyika tarehe 3-4/05/2024 ambao utakuwa na agenda ya kuchagua Askofu mpya wa Synod hiyo baada ya Askofu aliyepo Dkt. Davenport kumaliza muda wake.

Kabla ya Mkutano Mkuu Baba Askofu Dkt. Msafiri Mbilu pamoja na Msaidizi wake Dean Michael Kanju, wamepata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo: Kituo cha Katiba ya Marekani Philadelphia, ikumbukwe kuwa Katiba ya Marekani ndiyo Katiba kongwe kuliko katiba zote duniani ambayo ni ya tangu mwaka 1789.

Pia wameshiriki Bible Study ya Kanisa hilo ambapo Wachungaji wanakutana kuchambua neno la Mungu ili kuweka mikazo ya kutoa tafsiri sahihi kwa pamoja. Wametembelea Chuo Kikuu cha Kanisa (United Lutheran Seminary) ambacho kinaandaa watumishi wa Kanisa, ambapo kwa asili yake Chuo hicho kilianza mwaka 1864. Wametembelea Ofisi Kuu ya Synod, Usharika wa Reformation Lutheran Church Media wenye urafiki na Usharika wa Pangani.

Tutaendela kuwaletea taaarifa mbalimbali juu ya ziara hii ya Baba Askofu na Msaidizi wake nchini Marekani ikiwemo Mkutano Mkuu ambapo Baba Askofu atapata nafasi ya kutoa neno la Salaam na Jumapili tarehe 05/05/2024, atahubiri katika Usharika wa St. Luke wenye uhusiano na Usharika wa Mikanjuni. Tuendelee kuombea ziara hii itakayomalizika tarehe 08/05/2024.

Baba Askofu akiwa katika Usharika wa Reformation Lutheran Church wenye uhusiano na Usharika wa Pangani na hapa alikutana na marafiki wengi waliowahi kutembelea Usharika wa Pangani miaka iliyopita. Usharika huu  unaongozwa na Wachungaji wawili.

Katika picha ni baada ya Harambee ya kuchangia kazi za huduma za Kanisa.

Mchungaji Peruci Butiku (wa kwanza kushoto ) amabye pia ni Mtanzania ndiye mwenyeji wa viongozi wetu katika ziara hii.

Bible Study St. Matthew's Church

Philadelphia Maeneo ya makumbusho ya Uhuru na Katiba ya Marekani. Mji wa Philadelphia ndio ulikuwa Mji Mkuu wa Marekani kabla ya kumamishiwa Washington DC.

Chuo Kikuu cha United Lutheran Seminary