Print
Matukio katika Picha Ibada ya Mazishi ya Marehemu, Mchungaji Daniel Elierehema Kilangilo Magogo.Mchungaji Mstaafu Daniel Magogo aliitwa mbinguni tarehe 16/05/2024 na tarehe 20/05/2024 imefanyika Ibada ya mazishi yake Iliyoongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania,Baba Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa. na mwili wa marehemu Mchungaji Mstaafu Magogo, umepumzishwa katika makaburi ya familia yaliyopo Kwesimu Lushoto.
  
KATIKA HISTORIA
KUZALIWA: - Marehemu Mch. Daniel Elierehema Kilangilo Magogo alizaliwa tarehe 16/09/1925. ELIMU YA MSINGI: - Alianza elimu ya msingi mwaka 1944 katika Shule ya Msingi Lushoto Extended Primary School. MIDDLE SCHOOL: - Alisoma Vugiri Middle School mwaka 1948 – 1951. KUBATIZWA: - Alibatizwa mwaka 1950 akiwa na miaka 25. ELIMU YA SEKONDARI: - Alisoma Tanga School mwaka 1952 hadi 1953.
 
KUANZA KAZI: - Alianza kazi ya Afisa Maendeleo Serikalini mwaka 1954 ambapo alikuwa mfanyakazi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Bomani. Miongoni mwa majukumu yake ilikuwa kushughulikia uchapishaji wa nyaraka mabalimbali za Ofisi. Mwaka 1957 katika majukumu yake ya afisa maendeleo akiwa Mlalo alipata nafasi ya kufanya kazi ya maandiko kwa kushirikiana na Askofu Heinrisch Waltenberg.
 
MASOMONI UJERUMANI: - Mwaka 1958 fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani lilimpatia nafasi ya kwenda masomoni nchini Ujerumani ambako alisomea masomo ya Theolojia, Historia na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Hamburg hadi mwaka 1962 alipomaliza masomo na kurejea Tanzania na kubarikiwa kuwa Mchungaji. Mwaka 1963 alipewa wadhifa wa kuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri la Usambara Digo, ambapo akiwa Katibu Mkuu pamoja na aliyekuwa Church President Mchungaji Elirehema Mwanga waliweka sahihi ya kuunganisha Kanisa la Kilutheri la Usambara Digo na Makanisa mengine sita kuanzisha KKKT.
 
Mwaka 1965 alichanguliwa kuwa Church President KKKT-DKMs hadi 20/03/1969 alipochaguliwa kuwa Askofu Mteule wa KKKT–DKMs wadhifa aliotumikia mpaka tarehe 31/12/1970. Katika kipindi hicho pia alichaguliwa kuwa Kamishina wa dawati la Afrika katika ofisi ya Makao makuu ya Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani huko Geneva – Uswisi. 1971 hadi 1972 alikuwa Katibu wa Idara ya Maandiko kwenye Ofisi ya makao makuu ya KKKT – Arusha. 1972 hadi 1980 alikuwa Mkurugenzi wa KKKT Radio Sauti ya Injili – Moshi.
1980 hadi 1985 alikuwa Mbunge wa Wilaya ya Lushoto ambapo akiwa Mbunge aliwahi kuwa mwakilishi katika Bunge la Jumuia ya Mandola. Pia katika kipindi hicho amewahi kuwa Mjumbe wa Bodi za Mashirika ya Uma, ikiwemo Twico na pia Mjumbe wa Baraza la Chuo cha Ardhi. 1986 – 1996 alikuwa Katibu wa Idara ya Maandiko KKKT makao makuu – Arusha. NDOA Mwaka 1957 alifunga ndoa na Bi. Anjalina Daudi Sozi na kujaliwa kupata watoto saba, Wakike 5, Wakiume 2, Wajukuu 19 na Vitukuu 10.
Uongozi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kupitia Ofisi ya Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, unaendelea kutoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu. Bwana ametoa na Bwana ametwaa Jina la Bwana na lihimidiwe.
Hits: 9856