Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ameiomba Serikali kuongeza jitihada katika uchunguzi wanaoufanya ili kuwabaini mapema na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote wa vitendo vya utekaji na mauwaji ya watu hapa nchini.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito huo tarehe 28-9-2024 wakati akitoa salamu kwa waumini wa KKKT-DKMs katika Ibada ya Kustaafu kwa heshima Mchungaji Ezekiel Andrea Mwarabu  iliyofanyika katika Usharika wa Hale Jimbo la Tambarare na kukazia kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kutenda ukatili kwa mwingine ikiwemo mauwaji.

Amesema kwa msaada wa Mungu na maombi Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itafanikiwa kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika matukio hayo yanayo ichafua nchi.

Katika hatua nyingine amewakumbusha watumishi wa KKKT-DKMs kuendelea kutumika kwa uaminifu na kutenda haki  katika wajibu wao kama walivyoapa wakati wa kuingizwa kazini jambo litakalowaongoza kuwa na mwisho mwema na kustaafu kwa heshima kama ilivyokuwa kwa Mch.Mstaafu Ezekiel Mwarabu aliyelitumikia Kanisa kwa miaka 29 .

Amesema pamoja na kutumika madhabauni lakini pia watumishi katika Kanisa wanapaswa kujishughulisha na shughuli nyingine halali za kiuchumi zitakazo saidia boresha hali zao za maisha bila kuharibu wito mkuu wa kumtumikia Mungu.

Ibada hii ya Kustaafu kwa Mchungaji Ezekiel Andrea Mwarabu pia ilihudhuriwa na Msaidizi wa Askofu Mch. Michael Mlondakweli Kanju, Katibu Mkuu wa KKKT-DKMs Mwl. Julius Madiga, Wakuu wa Majimbo, Wachungaji, Wainjilisti, Mashemasi na Washarika wawakilishi kutoka Majimbo yanayounda KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

 
UTUMISHI 28/09/2024 MCHUNGAJI MWARABU alibarikiwa kuwa Mchungaji na Askofu Dkt. Erasto Kweka wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini, Aprili 25, 1993 katika Usharika wa Kana-Tanga. Hadi kustaafu kwake Mchungaji Ezekieli Mwarabu amekuwa mtumishi wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa miaka 29.
 
1987 – Mwalimu wa Elimu ya Kristo Usharika wa Korogwe.
1991 – Mazoezi (Internship) Usharika wa Korogwe.
1993 – Oktoba 1994 Mwalimu wa Shule ya Biblia Vuga.
Novemba 1994 – Aprili 1996 Usharika wa Malibwi
Mei 1996 – 9/9/2001 Usharika wa Ng’wangoi
9/9/2001 – 9/9/2010 Usharika wa Amani.
9/9/2010 – 07/01/2016 Usharika wa Pangani.
7/01/2016 – 4/12/2019 Usharika wa Hengiti.
4/12/2019 – 05/02/2020 Usharika wa Kwabada.
05/02/2021 – 10/05/2022 Usharika wa Mlingano.
10/05/2022 – 04/01/2023 Usharika wa Hale.