Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt Msafiri Joseph Mbilu, amewapongeza Washarika wa Usharika Mombo kwa namna wanavyoendelea kujitoa katika kumtumikia Mungu katika kuchangia ulipaji wa deni la Dayosisi pamoja na ujenzi wa Kanisa jipya na la kisasa linaloendelea kujengwa katika Usharika huo.

Ameyasema hayo wakati akitoa salamu zake katika Ibada ya Kipaimara iliyofanyika tarehe 12/10/2024 katika Jimbo la Tambarale Usharika wa Mombo na kuongeza kuwa amefarijika kuona Washarika wa Usharika wa Mombo wanavyojitoa katika kuchangia ulipaji wa deni la Dayosisi na anaamini kwa namna ambavyo kila mmoja anajitoa siku moja deni hilo litakwisha huku akiwasihi kila mmoja kuendelee kujitoa kwa moyo.


Amewasihi Washarika hao kuendelea kujitoa ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo kwani kwa kufanya hivyo watabarikiwa na Mungu.Pia Askofu Dkt Mbilu ameunga mkono ujenzi wa Kanisa hilo kwa kutoa kiasi cha Tsh 200,000/=

Wakati akihubiri katika Ibada hiyo, Askofu Dkt Mbilu amewataka waumini kuendelea kuweka Imani yao kwa Mungu huku wakiendelea kumtegemea Mungu katika maisha yao kwani kwa kufanya hivyo hiyo ndiyo Imani ya kweli na wasikubali kuyumbishwa na mafundisho potofu ambayo yameibuka kwa wingi katika nyakati hizi.

Katika hatua nyingine Askofu Dkt. Mbilu amewataka Washarika kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akiwataka Washarika hao kujitokeza katika kujiandikisha katika Daftari la kudumu la Wapiga kura,Wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wafanye hivyo na siku ya kupiga kura watu wajitokeze kwa wingi ili wakachague viongozi wazuri.

Nao Vijana waliobarikiwa katika Ibada hiyo wakitoa itikio baada ya kubarikiwa kupitia Risala yao wamemshukuru Askofu Dkt. Mbilu pamoja na wote waliohusika kuwafundisha neno la Mungu kwa usahihi huku wakiahidi kuishika imani ya Kristo bila kuyumbishwa na mafundisho yoyote potofu pamoja na kuyafanyia kazi yote waliojifunza kwa kipindi cha miaka miwili.

Jumla ya Vijana 92 walibarikiwa katika Ibada hiyo huku wawili kati yao wakibatizwa. Vijana hao walitoa kiasi cha Tsh 450,000/= kwaajili ya kuunga mkono juhudi za kulipa deni la Dayosisi ambapo baada ya kuungwa mkono na Washarika, kilipatikana kiasi cha Tsh 2,625,550/= huku ahadi ikiwa ni Tsh 100,000 na kufanya jumla ya kiasi cha Tsh 2,725,550/= ambazo zitaelekezwa katika kulipa deni la Dayosisi.