Viongozi wa Dini mbalimbali kupitia kamati ya amani Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wamekutana leo Octoba 15, 2024 ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu amani katika jamii hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakao fanyika Novemba 27, 2024 na kuhamasisha jamii kushiriki katika Uchaguzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Zephania Sumaye ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Utondolo Lushoto ameipongeza kamati hiyo kwa kusadifu madhumuni ya uwepo wake na kuwaeleza kuwa ipo haja ya kukaa pamoja ili kuona namna bora ya kutekeleza mipango mikakati iliyonayo ikiwemo suala la kupambana na ushoga.
Awali mwenyekiti wa Kamati ya Amani Wilaya ya Lushoto ambae pia ni Msaidizi wa Askofu KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMS) Mch. Michael Kanju amesema kuwa uwezeshwaji katika masuala ya kifedha ili kuweza kuzifikia jamii za maeneo ya ndani zaidi na kukosa ofisi imekuwa ni changamoto kubwa inayoikabili kamati hiyo katika kufikia malengo yake.
Nae Katibu wa Kamati hiyo ambae pia ni katibu wa BAKWATA Wilaya ya Lushoto, Mohamed Said Baruti ameiomba serikali kusaidia mchakato wa kushusha majukumu ya kamati hiyo hadi kufikia ngazi ya tarafa na kata ili iweze kufahamika hatua itakayo ondoa mtazamo hasi kwa baadhi ya watu kuhusu kamati hiyo.
Ili kukabiliana na changamoto ya kukosa ofisi Mkuu wa Wilaya ya Lushoto alimuomba Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Lushoto Ali Daffa kuona uwezekano wa kulitafutia ufumbuzi changamoto hiyo ambapo aliahidi kufanyia kazi kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Lushoto na kuhusu kuishusha kamati ngazi ya chini Dc Sumaye ameahidi kulitekeleza baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kukamilika.
Mlezi wa Kamati ya amani Wilaya ya Lushoto Askofu wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs) Mch Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, aliwasihi viongozi hao kuendelea kushikamana ili kuwaletea wananchi amani ya kweli itakayo saidia kusukuma ajenda ya maendeleo kwa taifa na wananchi wake hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Kamati ya Amani Wilaya ya Lushoto inaundwa na viongozi wa dini mbalimbali ambapo kwa pamoja wanashirikiana kuhakikisha kunakuwepo na haki, upendo, amani na umoja kwa dini zote Tanzania na wananchi wake.