Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt Msafiri Joseph Mbilu, amesema kuwa mwamko wa elimu katika Shule ya Sekondari Lwandai pamoja na Bangala Lutheran Junior Seminary ambazo zote zinamilikiwa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, umeongezeka zaidi ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali na kuwaomba wazazi na walezi kupeleka watoto wao katika Shule hiyo.
Ameyasema hayo wakati alipokua akizungumza na wazazi pamoja na walezi katika Mahafali ya 35 ya kidato cha nne yaliyofanyika tarehe 19/10/2024 katika Shule ya Sekondari Lwandai, ambapo amesema kuwa alipochaguliwa kuiongoza KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Novemba 2020, alitaka kujua hali ya Shule hizo ikoje ndipo alipopokea taarifa ya kuwa Shule ya Sekondari Lwandai ina wanafunzi 8 wa kidato cha kwanza huku Shule ya Bangala iliyoko Soni Halmashauri ya Bumbuli Wilaya ya Lushoto ikiwa na wanafunzi 3 pekee hali ambayo ingesababisha kufungwa kwa Shule hizo.
Ameongeza kuwa kwa hali hiyo ndipo alipoitisha Kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi kilichoketi Novemba 2020 na kuja na maazimio ya kila Usharika wa KKKT-DKMs usomeshe Mtoto mmoja kulingana na idadi ya Sharika wakati huo kuwa 60 hivyo jumla ya Wanafunzi 60 kutoka Sharikani walipatikana ambapo waligawanywa 30 katika Shule ya Sekondari Lwandai na wengine 30 Shule ya Bangala jambo ambalo lilipekea shule hizo kurudi katika hali nzuri na hapa akawashukuru Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT-DKMS kwa uamuzi huu mzuri.
Hata hivyo Askofu Dkt. Mbilu amewashukuru Washarika kupitia Sharika zote za KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, kwa kujitoa kwao kwa mali zao kuwasomesha vijana hao huku akiwataka vijana hao 50 watakao hitimu mwaka huu kusoma kwa bidii kwani bidii katika masomo ndio zitakazo pelekea kufanya vizuri katika mitihani yao na kupata sifa za kujiunga na kidato cha tano kwani Dayosisi kupitia Sharika zake itaweka mpango ili wanafunzi hao watakao fanya vizuri waendelee kusomeshwa na Sharika kidato cha 5 na 6.
Aidha Askofu Dkt. Mbilu ametoa wito kwa Wazazi na Walezi kuwapeleka vijana wao katika Shule hizo kwani kwa sasa kuna walimu wazuri na wenye uzoefu wa kutosha kumfanya mtoto aweze kufanya vizuri, Pia amesema shule hizo zinalea na kukuza vipaji mbalimbali vya watoto ikiwemo muziki ambapo katika shule hizo wengi wameendelea kujifunza huku akitoa zawadi ya tarumbeta moja,pia Askofu Dkt.Mbilu alitoa zawadi ya kalamu kwa wahitimu kama alama ya kuwatakia baraka za Mungu na mafanikio katika mitihani yao ya kidato cha nne itakayo fanyika tarehe 11 Novemba hadi tarehe 29 Novemba 2024
.