Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewasihi Wanawake kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza katika jamii na Kanisa kwaajili ya kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na umasikini pamoja na utegemezi.
Askofu Dkt. Mbilu ameyasema hayo leo Oktoba 23,2024 katika ufunguzi wa kongamano la wanawake ukanda wa Afrika linalojumuisha Wanawake wawakilishi kutoka Dayosisi nne ambazo ni wanachama wa UEM linalofanyika katika Taasisi ya Elimu ya Kolowa Technical Training Institute (KOTETI) iliyopo Magamba Wilayani Lushoto.
Kongamano hili linalodhaminiwa na UEM lina la lengo la kuwajengea uwezo wanawake namna ya kujishughulisha katika kazi mbalimbali zitakazowafanya wajikwamue katika nyanja zote za kijamii ikiwemo masuala ya kiuchumi.
Aidha, Askofu Dkt.Mbilu amesema njia moja wapo ya kujikwamua na umaskini ni kufanya kazi kwa bidii hivyo ni vyema kuwajengea wanawake uwezo wa kufanya kazi mbalimbali zitakazowasaidia kimaisha kwani ukimuwezesha mwanamke ni sawa na kuiwezesha jamii nzima.
Kwaupande wake Dkt. Mary Mbilu mmoja wa washiriki na muwezeshaji (facilitator) wa Kongamano hilo akishirikiana na Thea Hummel kutoka Wuppertal Ujerumani anayesimamia kitengo cha Wanawake katika UEM,amesema kuwa baada ya kupata mafuzo hayo atawashirikisha wanawake wengine katika ngazi ya Sharika na jamii ili kila mwanamke awe na uwezo na ujuzi wa kuchangamkia fursa zitakazomsaidia kimaisha, huku akiwataka wanawake kujiimarisha kiuchumi punge fursa zinapopatikana ili kutimiza malengo na shabaha zao katika kutatua changamoto za wanawake katika jamii sambamba na kuwafungamanisha katika fursa za kujikwamua na umasikini na kujiletea maendeleo endelevu.
Nao baadhi ya wanawake wanaoshiriki kongamano hilo la siku 3 wameushukuru uongozi wa UEM kwa kuandaa kongamano hilo litakalowajengea uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowafanya kutokuwa tegemezi katika familia na kuahidi kwenda kutoa elimu watakayoipata katika jamii mara baada ya mafunzo hayo yanayoendeshwa na Mratibu wa kitengo cha wanawake UEM, Thea Hummel.
UEM: United Evangelical Mission ni chama Cha kiinjili Cha kimisioni kilianzishwa mwaka 1996 na wamisionari kutoka Ujerumani wa Rhenish na Betheli ambao walifika Africa, na Asia kwa ajili ya kuanzisha shughuli za Dini. Katika Africa walifika katika nchi 7 ambazo ni Tanzania, DR Congo, Africa ya Kusini, Botswana, Cameroon, Namibia na Rwanda kukiwa na madhehebu 15. Katika Tanzania inawakilishwa na Makanisa 4 ya KKKT ambayo ni KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na KKKT Dayosisi ya Karagwe.
 
#Awali washiriki wa Kongamano hilo walishiri Ibada ya Asubuhi pamoja na kuitembelea Ofisi Kuu ya KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMS) yenye Makao Mkuu Wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga pamoja na kusaini kitabu cha wageni katika Ofisa ya Askofu KKKT-DKMS.