Ikiwa leo tarehe 27/10/2024, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, ni Siku ya Kukumbuka Matengenezo ya Kanisa (Reformation) Askofu Dkt. Mbilu amesema kuwa Kanisa litaendelea kukemea mafundisho potofu yaliyotanda katika ulimwengu na kuendelea kusimama katika msingi wa kuihubiri kweli ya Kristo.
Askofu Dkt. Mbilu, ameyasema hayo leo tarehe 27/10/2024 wakati akihubiri akiwa katika Jimbo la Kusini Usharika wa Mamba na kuongeza kuwa Wakristo wanapaswa kusimama katika kweli ya Kristo kwani wapo wanaodanganywa na kufuata mafundisho potofu yanayo waaminisha watu kuwa hata pasipo kufanya kazi wanaweza kuombewa na kupata utajiri jambo ambalo Askofu Dkt. Mbilu amewataka Wakristo kupinga na kujiweka mbali na mambo hayo na kuwasihi kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwani kwa njia hiyo ndio njia pekee itakayo wawezesha kupata utajari na mafanikio katika maisha.
Ameongeza kuwa Dkt. Martin Luther alisimamia ukweli wa neno la Mungu katika kupambana na mafundisho potofu yaliyofanya wokovu ufikie hatua ya kununuliwa kwa hela kupitia vyeti vya msamaha vilivyo halalisha maovu ikiwemo kufutiwa dhambi.Katika hili Dkt. Martin Luther alisimama na kuweka wazi kuwa Neno la Mungu linatosha na halihitaji msaada wowote na hapa akawa tayari kufa kwa ajili ya ukweli pale aliposema “Hapa nasimamia ukweli wa neno la Mungu, sitabadili msimamo, nisaidie Mungu wangu”.
“Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kila Jumapili ya kila mwaka mwishoni mwa mwezi wa kumi karibu na tarehe 31 huadhimisha sikukuu ya matengenezo ya Kanisa yaliyofanyika tarehe 31/10/1517 lengo likiwa kurudisha mafundisho sahihi ya neno la Mungu yasiyopunguzwa sehemu yoyote.Alisema Askofu Dkt. Mbilu.
Dkt. Martin Luther, Baba wa matenegenezo ya Kanisa aliyekuwa na lengo la kurekebisha na kutengeneza baadhi ya mafundisho na taratibu zilizokuwa zikifanywa na Kanisa la wakati ule Kanisa la Kirumi ambazo zilikuwa hazijengwi kwenye msingi wa Neno la Mungu ili kurejea katika msingi wa Kibiblia.
Pamoja na hayo Baba Askofu Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, akiwa katika Jimbo hili la Kusini linaloongozwa na Mch. Issai Mweta, kulikuwa na matendo mbalimbali ikiwo kubarikiwa kwa Vijana wa Kipaimara wapatao 144 na 2 kati yao kubatizwa na awali Ibada hii ilitanguliwa na Ibada ya uwekwaji wa Jiwe la Msingi wa Kanisa la Mtaa wa Kwesine.