Shule za Sekondari za Lwandai na Bangala Junior Seminary, zinazomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), zimeendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika November, 2024
Katika matokeo hayo, shule ya Lwandai imevutia zaidi baada ya kutoa mwanafunzi aliyepata alama za juu akiwa na daraja la kwanza lenye pointi saba (One ya 7), kitu kinachoashiria uwekezaji mkubwa katika elimu bora na juhudi za walimu pamoja na wanafunzi.
Kufuatia matokeo hayo Askofu wa KKKT-DKMs, Dkt. Msafiri Joseph Mbilu ,ametoa pongezi kwa walimu na wafanyakazi wa Shule hizo kwa kazi nzuri walioifanya huku akiahidi kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuweka msingi imara wa mafanikio zaidi ya siku zijazo.
Kakita hatua nyingine Askofu Dkt. Mbilu, ametoa shukrani zake za dhati kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Dayosisi kwa kukubali ombi la kila Usharika wa KKKT-DKMS kusomesha mwanafunzi mmoja katika Shule hizi.
“ninapoyatazama matokeo haya ya kishindo ya Shule zetu Lwandai na Bangala ninajikuta mdomo wazi nikimshangaa Mungu kwa jambo hili kubwa alilotutendea. Ninawapongeza ninyi wote kwa maamuzi yale magumu tuliyofanya kwenye kikao chetu cha kwanza cha tarehe 17.12.2020 kuwa kila Usharika usomeshe mwanafunzi mmoja kuanzia Januari 2021 ili kuondoa aibu ya Shule hizi kuwa na wanafunzi wachache wa kidato cha kwanza Lwandai 8 na Bangala 3. Hili limezaa matunda haya na kwa hakika Shule zetu zimefufuka. Hongereni sana.
Siku chache kabla ya Mtihani wa kidato cha Nne nilitembelea Shule zetu hizi kufanya maombi na watoto wetu na kuwapa kila mmoja kalamu ya kufanyia Mtihani kwa niaba yenu. Hakika Mungu amesikia maombi yetu na ametenda na ameamua KUTUPA RAHA. Nawapongeza ninyi Wajumbe wa Halmashauri Kuu, Wana KKKT-DKMS na wadau wote wa maendeleo kwa Ufadhili wao.
Nawapongeza Wazazi wa watoto hawa, Nawapongeza Wakuu wa Shule zetu, Walimu wote na watenda kazi wote kwa ufaulu huu wa hali ya juu sana. Tunazo hadi Divisheni One ya point 7. Nawapongeza watoto wetu kwa kufanya vizuri kwenye Mtihani Huu”Amesema Askofu Dkt. Mbilu.
Pamoja na hayo Askofu Dkt. Mbilu, amempogeza kipekee mwanafunzi Helena Frank Kaduma wa shule ya sekondari Lwandai kwa kupata ufaulu wa Division One ya point 7 ambapo mwanafunzi huyo amesomeshwa na Usharika wa Hale pamoja na mwanafunzi kutoka shule ya seminari ndogo ya Kilutheri Bangala,Dickson David Kika ambaye amepata ufaulu wa Division one ya 9 ambaye amesomeshwa na usharika wa Soni.
Matokeo haya mazuri yanaendeleza sifa nzuri ya shule hizi kama vituo vya elimu vinavyozalisha viongozi wa kesho walio na maarifa na maadili mema, na ujuzi unaohitajika kwa maendeleo ya Taifa. Sharika za KKKT-DKMS zitaendelea kuwasomesha vijana hawa kidato cha Tano na cha Sita. Mungu aendelee kutubariki tunapoyafanya makubwa haya. "BWANA AKASEMA, USO WANGU UTAKWENDA PAMOJA NAWE, NAMI NITAKUPA RAHA"(Kutoka 33:14).