![]()
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ametoa pongezi za dhati kwa Wainjilisti Wanaume wa Dayosisi kwa huduma yao na uaminifu katika kuitenda kazi shambani mwa Bwana.
Akizungumza tarehe 28/11/2025 wakati akifungua semina maalum inayowakutanisha Wainjilisti wanaume wa KKKT-DKMs katika Usharika wa Korogwe, Askofu Dkt. Mbilu alisisitiza kuwa uongozi wa Dayosisi unatambua, kuthamini na kulinda mchango muhimu wa Wainjilisti katika kukuza na kuimarisha kundi la Mungu.
Aliongeza kuwa nguvu, hekima na kujitoa kwao kunaleta matokeo na ustawi si tu katika Kanisa bali hata katika jamii wanazozihudumia.
Kwa msisitizo wa kipekee Askofu Dkt. Mbilu ameonesha moyo wake wa kujali watumishi kwa kubainisha kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu masuala yote yanayohusu ustawi na haki za watumishi wote katikadayosisi.
Ameahidi kuhakikisha stahiki mbalimbali zinaendelea kutolewa kwa wakati, ikiwemo michango ya NHIF na mifuko mingine ya kijamii, ili watumishi waendelee kufanya kazi kwa amani, uadilifu na matumaini huku akiitaka Ofisi ya Msaidizi wa Askofu kutoa mapema taarifa katika Ofisi ya Askofu punde Wainjilisti wanapokaribia kustaafu.
Askofu Dkt. Mbilu amesisitiza kuwa uongozi hauishii katika kuongoza tu, bali unajumuisha pia kuhakikisha kuwa wale wanaohudumu katika nafasi mbalimbali katika Dayosisi wanatunzwa, wanathaminiwa na kuwekewa mazingira bora ya kutekeleza huduma ikiwa hii ni sehemu ya wito wa Kristo wa kujenga, kuenzi na kutiana nguvu katika kuitenda kazi ya Bwana.
Tufuatilie kwenye mitandao yetu ya kijamii
INSTAGRAM - / elctned
FACEBOOK ACCOUNT North Eastern Diocese
FACEBOOK PAGE - ELCT-North Eastern Diocese
YOUTUBE - / KKKT DKMS Online TV
WEBSITE: www.elctned.org
KWA MAONI NA USHAURI:
Simu : +255 743 399 798