Print

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, amewashukuru kwa dhati wanadayosisi wote kwa namna wanavyoendelea kujitoa katika ulipaji wa Deni la Dayosisi, akisisitiza kuwa hatua hiyo imekuwa ikitoa matumaini makubwa katika kufanikisha mpango wa kulimaliza deni hilo.

Askofu Dkt. Mbilu ametoa shukrani hizo katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika tarehe 07 Desemba 2025 katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto, ibada iliyoambatana na matukio mbalimbali muhimu ya kiimani na kiuongozi. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na kubarikiwa kwa Vijana wa Kipaimara pamoja na kuwaingiza kazini Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya KKKT–DKMs.

Aidha, Askofu Dkt. Mbilu alisisitiza kuwa njia madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya deni ni kila msharika na kila usharika kutimiza wajibu wake wa kuchangia Deni la Dayosisi kama walivyopangiwa huku akibainisha kuwa utayari wa washarika na wadau wa maendeleo ni ishara njema ya umoja na uwajibikaji katika kulikabili Deni hilo huku akimpongeza MCH. ANNA TULLO MSISILI pamoja na Washarika wa Usharika wa Ubiri ambao wao wamemaliza kiwango chao cha uchangiaji wa Deni la Dayosisi.

Katika hatua nyingine, Askofu Dkt. Mbilu alifunga rasmi kalenda ya matukio ya Dayosisi kwa mwaka huu, huku akitoa shukrani kwa viongozi wa Kanisa, sharika zote, vituo vya kazi na waumini kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika ziara zake ndani na nje ya Dayosisi.

Katika Ibada hiyo, jumla ya Vijana 34 walibarikiwa, huku 2 kati yao wakibatizwa. Kwa kuunga mkono jitihada za Dayosisi katika kulipia deni, vijana hao pamoja na wazazi, walezi na waumini walioshiriki katika Ibada hiyo walitoa mchango wa jumla ya Tsh. 1,411,300.

 

 

Hits: 1211