Print

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki (KKKT-DKMs), Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ametoa wito kwa viongozi, wakuu wa vituo pamoja na watumishi wote waliokabidhiwa jukumu la kusimamia mali za Dayosisi kuhakikisha wanatunza, wanalinda na kuendeleza kwa hekima.
Askofu Dkt. Mbilu amesema kuwa mali za kanisa ni amana kutoka kwa Mungu, hivyo zinapaswa kusimamiwa kwa hofu ya Mungu, uwazi, uadilifu na nidhamu ya hali ya juu ili kudumisha imani hata kwa marafiki na wadau wengine mbalimbali wa maendeleo ambao kwa namna moja ama nyingine wameonesha moyo wa kuisaidia Dayosisi.
 
Ameyasema hayo Desemba 16, 2025, wakati wa Ibada ya kuweka wakfu gari jipya aina ya Land Cruiser, iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Dayosisi. Katika ibada hiyo, Askofu Dkt. Mbilu, aliwashukuru kwa dhati marafiki wa Dayosisi kutoka Bethel, Ujerumani, na kwa namna ya kipekee Familia ya Bw.Werner Jakob Blauth na mkewe Barbara Blauth, kwa mchango wao mkubwa uliowezesha kupatikana kwa gari hilo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa KKKT-DKMs, Mwl. Julius Samwel Madiga, amemhakikishia Askofu Dkt. Mbilu, kuwa gari hilo litatunzwa vizuri na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa kwa maslahi mapana ya kituo. Aidha, Mkuu wa Kituo cha Afya ya Akili cha Lutindi Mental Hospital, Dkt. Marwa, ameushukuru uongozi wa Dayosisi pamoja na marafiki kutoka Bethel kwa kuwezesha upatikanaji wa chombo hicho muhimu cha usafiri.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Jamii wa Dayosisi, Mwl. Afizai Vuliva, alimpongeza Askofu Dkt. Mbilu kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ushirikiano ambayo yamevutia marafiki wa Dayosisi na kuwahamasisha kujitoa katika kuchangia maendeleo ya huduma mbalimbali ndani ya Dayosisi.

Hits: 1055