Print

Askofu wa KKKT-Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,Dkt. Msafiri Joseph Mbilu, ameongoza kikao kazi cha Wachungaji kilicholenga kuweka mipango yamwaka 2026 na kufanya tathmini ya hali ya Deni la Dayosisi pamoja na kuweka mikakati mipya ya pamoja ya kulikabili na kulimaliza.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 13 Januari, 2026 katika Usharika wa Kanisa Kuu Lushoto, kikihusisha Wachungaji kutoka sharika mbalimbali za Dayosisi. Lengo kuu la kikao kilikuwa ni kuimarisha ushirikiano, kuweka mikakati shirikishi,kupanga na kuendeleza mipango ya utekelezaji kwa mwaka 2026, ikiwemo mpango mahsusi wa kumaliza deni la Dayosisi.

Akifungua kikao hicho, Askofu Dkt. Mbilu aliwashukuru kwa dhati Wachungaji, watumishi na Washarika wote wa Dayosisi kwa moyo wa kujitoa na ushiriki wao mkubwa katika kuitenda kazi ya Bwana, hususani katika kuchangia deni la Dayosisi. Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa waaminifu, na watu wenye mshikamano na  maono ya pamoja kwa maendeleo ya Kanisa.

 Katika kikao hicho pia kulifanyika zoezi la utoaji wa tuzo ya pongezi kwa moja ya usharika uliofanya vizuri katika uchangiaji wa deni la Dayosisi. Uongozi wa Dayosisi ulimpongeza kwa kipekee Mch. Anna Msisili wa Usharika wa Ubiri pamoja na washarika wa Usharika huo, ambao wamefanikiwa kukamilisha kiwango chote cha uchangiaji wa deni la Dayosisi na kushika nafasi ya KWANZA kati ya sharika 76 za Dayosisi kwa kutimiza lengo kwa wakati.Zoezi hili lilifanyika katika sehemu ya ufunguzi wa kikao hicho.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mchungaji  Anna Msisili, aliyeambatana na Wazee wa Kanisa wa Usharika huo.Tuzo hiyo ni miongoni mwa tuzo zinazotolewa kwa sharika 10 za mwanzo zitakazokamilisha deni kwa wakati, na inabeba ujumbe wa neno la Mungu kutoka Kutoka 33:14 unaosema: “Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.”

Aidha, taarifa ya kina kuhusu hali ya uchangiaji wa deni la Dayosisi kwa kila usharika iliwasilishwa kwa Wachungaji na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Dayosisi, CPA Peter John Singano. Ilielezwa kuwa taarifa rasmi kwa Washarika wote itatolewa tarehe 18 Januari, 2026, na itasomwa katika sharika.

Hits: 937